"MSHIKAKI" WAUA WANAWAKE WAWILI KAHAMA
Wanawake wawili wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wameipanda kwa mtindo wa “Mshikaki”
kuanguka kutokana na mwendokasi wa mwendeshaji katika eneo la Zongomela
Mbugani kata ya Zongomela wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa
Shinyanga,ACP Simon Haule ajali hiyo imetokea jana Aprili 3,2018 saa
moja na dakika 45 usiku katika barabara ya kuelekea Nyandekwa pikipiki
ikitoka kijiji cha Igunda kuelekea Kahama Mjini.
Amesema pikipiki hiyo yenye namba za
usajili T.185 CJF aina ya Sanlg mali ya mtu asiyefahamika,ikiendeshwa
na dereva asiyefahamika ilianguka na kusababisha vifo vya wanawake
wawili.
Amewataja waliopoteza maisha katika
ajali hiyo kuwa ni Mwanaisha Kabichi Maganga (32) mkazi wa Nyasubi na
Zawadi Stanley (28) mkazi wa Nyihogo ambao walikuwa wamebebwa kwenye
pikipiki hiyo.
“Chanzo cha ajali ni mwendokasi wa
mwendesha pikipiki ambaye pia yeye na abiria wake hawakuzingatia
sheria,taratibu,kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa kila mara
kupiga vita na kukataza upakiaji/upandaji wa abiria wawili kwenye
pikipiki moja ya magurudumu mawili maarufu kama “Kupakia mishikaki”,amesema Kamanda Haule.
Ameongeza kuwa juhudi za kumtafuta
mwendesha pikipiki aliyekimbia baada ya ajali na kwamba miili ya
marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika
hospitali ya mji wa Kahama.
