CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA KAGERA (KCU) CHAFAFANUA KUHUSU MALIPO YA AWALI YA KAHAWA YA WAKULIMA
Mwenyekiti
wa Bodi ya Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg Onesmo
Niyegila (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa
ufafanuzi kuhusu malipo ya awali ya kahawa ya wakulima wa Chama Kikuu
cha Kagera KCU (1990) Ltd, Leo 7 Aprili 2018, Mwingine ni Kaimu meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg John kanjagaile. Picha Zote Na Mathias Canal, WK
Waandishi
wa habari wakifatilia Mkutano wa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha
ushirika cha Kagera (KCU) Ndg Onesmo Niyegila wakati akitoa ufafanuzi
kuhusu malipo ya awali ya kahawa ya wakulima wa Chama Kikuu cha Kagera
KCU (1990) Ltd, Leo 7 Aprili 2018, Katika Ukumbi wa Ofisi za Wizara ya
Kilimo (Kilimo 4).
Na Mathias Canal, WK-Dodoma
Mwenyekiti
wa Bodi ya Chama Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU) Ndg Onesmo
Niyegila ametoa ufafanuzi kuhusu malipo ya awali ya kahawa ya wakulima
wa Chama Kikuu cha Kagera KCU (1990) Ltd kama ilivyojadiliwa kwenye
Mkutano wao Mkuu tarehe 27/03/2018.
Amebainisha
hayo wakati akizingumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Mjini
Dodoma na kusema kuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera si Kampuni ya
kununua kahawa bali ni ushirika wa wakulima wadogo wadogo wenye lengo la
kuunganisha nguvu zao kwa pamoja katika kuhudumia zao la kahawa na kuliwasilisha sokoni kwa utaratibu wenye tija endelevu na kisha kugawana mapato baada ya kufanya mauzo.
Alisema bei halisi ya mkulima kwa upande wa Ushirika inapatikana mara baada ya mauzo ya kahawa kufanyika ambapo wakulima
hulipwa malipo ya mwisho kwa kadri ya bei ya kuuzia iliyopatikana
sokoni na hesabu ya mwisho kuwasilishwa kwenye mkutano mkuu.
Hivyo
kwa vile mchakato wa mauzo huchukua si chini ya kipindi cha mwezi mmoja
tangu mkulima awasilishe kahawa yake kwenye ushirika hadi malipo ya
mwisho kufanyika, basi ili kumuondolea mkulima adha ya kusubiri malipo
yake yote baada ya mauzo wakati anahitaji kujikimu na kukidhi mahitaji
yake muhimu, wakulima wenyewe kwa utashi wao kupitia Mkutano Mkuu, wanajadili malipo ya awali atakayotanguliziwa mkulima wakati anasubiri malipo ya mwisho.
Niyegila
alibainisha kuwa mnamo tarehe 27/03/2018, Chama Kikuu cha Kagera
kilifanya Mkutano wake Mkuu ambao pamoja na mambo mengine wanachama
walijadili malipo ya awali ya mkulima (Advance Payments). Katika makisio
hayo, Menejimenti na Bodi ya KCU (1990) Ltd walipendekeza malipo ya awali yawe ni TZS 1,000 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda.
Alisema
kuwa baada ya mjadala, wanachama waliagiza kupitiwa upya kwa makisio
hasa katika upande wa malipo ya awali na kuangalia namna ya kupandisha
kiwango cha malipo ya awali. Aliongeza kuwa Kiwango kipya pendekezwa
kitawasilishwa kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini kwa ajili ya
kuidhinishwa.
Alisisitiza
kuwa kile kilichojadiliwa kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama si tangazo
la bei bali ni malipo ya awali kwa mkulima ambapo Kwa mujibu wa sheria,
bei elekezi ya zao la kahawa inatolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania kwa
utaratibu wa ushirika, bei halisi itajulikana mara baada ya mauzo ya
kahawa kufanyika sokoni na si vinginevyo.
Niyegila
aliongeza kuwa kwa utaratibu wa sasa wa Serikali, kahawa yote
itakusanywa kupitia kwenye Vyama vya Ushirika na kupelekwa sokoni
Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo wanunuzi wote watanunulia
hapo mnadani.
Kwa mantiki hiyo, hakuna mkulima yeyote atakayeruhusiwa kuuza kahawa nje ya mfumo wa ushirika
MWISHO.