MKWASA AFUNGUKA KUHUSU KUACHIA NGAZI YANGA

Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwasa,
ametolea ufafanuzi uwepo wa taarifa zinazoeleza kuwa wadhifa wake
umekalia kuti kavu.
Mkwasa alisema kuwa hakuna tatizo lolote lililopo ndani ya klabu, bali ni mitandao tu imekuwa ikiandika kila wanalolijua.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya kuenea kwa taarifa
zinazoeleza kuwa Mkwasa anaweza akaachia ngazi ya Ukatibu Mkuu ndani ya
Yanga, baada ya kuhusishwa na kuondoka kwa Kocha George Lwandamina.
Kupitia kipindi cha Michezo cha EFM Radio, jana jioni,
Katibu huyo pia alisema Yanga imeshakuwa na viongozi wengi, yeye si
Katibu wa kwanza kuanza kazi pale, walikuwepo wengi na wakaondoka.
"Mimi si mtu wa kwanza kuwa Katibu Mkuu Yanga, walikuwepo
wengi waliokalia kiti hiki lakini hawapo kwa sasa, kama wakati wangu
ukifika wa kuondoka, nitaondoka na atakuja mwingine" alisema Mkwasa.
Mbali na hayo, Mkwasa amewataka Wanayanga wote kuwa
watulivu katika kipindi hiki ili kuepusha ujio wa migogoro ambayo
inaweza ikaleta mtafaruku ndani ya klabu, ambapo hivi sasa wanasubiri
mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolaiita Dicha FC.