ZITTO KABWE AGUSWA NA KILIO CHA WAFANYABIASHARA WA SAMAKI MWANZA, ATOA RAI KWA RAIS MAGUFULI.
Mbunge wa Kigoma mjini ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ACT
WAZALENDO Mhe. Zitto Kabwe, asubuhi ya leo Januari 28, 2018 ameonyesha
kuguswa na kilio cha wafanyabiashara wa samaki jijini Mwanza.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Zitto amemkumbusha Mhe. Rais
Magufuli kuhusu adha ya uliopaji kodi wanayokumbana nayo
wafanyabiashara hao kwa samaki wanaosafirishwa kwenda kwenye mikoa ya
mpakani mwa nchi kutoa mwaloni Kirumba jijini Mwanza.
Mhe. Zitto amenukuu kichwa cha habari cha gazeti moja la mtandaoni na
kisha kuwatag Mheshimiwa Rais Magufuli na viongozi wengine, pamoja na
vyombo kadhaa vya habari ili kufikisha ujumbe wake huo.
“RAIS MAGUFULI TUSAIDIE: WAFANYABIASHARA WA SAMAKI MWANZA WALIA” ametweet Zitto akinukuu moja ya gazeti hapa nchini.
Wafanyabiashara wa samaki katika soko la mwaloni Kirumba jijini
Mwanza, kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakilalamikia utaratibu mpya
wa kulipia kodi samaki ambao wamekuwa wakisafirishwa kwenda kwenye
baadhi ya mikoa ambayo ipo mpakani mwa nchi.
Utaratibu huo mpya umeonekana kuwaathiri sana wafanyabiashara hao
jambo lililopelekea kutokea kwa migomo ya mara kwa mara ikiwahusisha
wafanyabiashara hao kushinikiza kuondolewa kwa utaratibu mpya huo ambao
unaonekana kuwanyonya.
Wafanyabiashara hao ambao idadi yao ni zaidi ya 2000, wamemuomba Mhe.
Rais Magufuli kusikia kilio chao hicho na kutatua mgogoro ambao
umekuwepo kwa muda sasa kati ya Ofisi ya Mkoa wa Mwanza, wawakilishi wa
wizara ya Uvuvi na Mifugo, pamoja na mamlaka ya mapato nchini yaani TRA.