Wawili mbaroni kwa wizi wa miundombinu ya TANESCO
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni linawashikilia watu wawili kwa
tuhuma za wizi wa miundombinu ya umeme yenye thamani ya milioni 61 ya
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Wakati
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu
Kamshna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, DCP Lucas Mkondya
amesema jana kikosi kazi cha kuzuia uharibifu wa miundombinu cha Tanesco
kwa kushirikiana na polisi baada ya kupata taarifa za wizi wa
miundombinu kutoka kwa raia wema.
Kilifanya upekuzi katika nyumba ya Wilfred Baruti mkazi wa Makumbusho na kukuta vifaa vya wizi vya kuunganishia umeme .
Pia kilifanya upekuzi katika nyumba ya Beatrice Emanuel mkazi wa Salasala na kukamata vifaa vya umeme.
DCP
Mkondya amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa
mahojiano na upelelezi utakapo kamilika watapelekwa mahakamani kwa hatua
zaidi za kisheria.
Pia
DCP Mkondya amesema Kikosi Maalumu cha Kupambana na Uhalifu cha kanda
ya Dar es Salaam kimekamata watuhumiwa wawili wakiwa na funguo bandia 75
kwa kosa la uvunjaji nyumba za biashara, maghala ya kuhifadhia bidhaa
na maduka.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ally Makwega mkazi wa Tandika na Fabian Greyson mkazi wa Yombo.