polisi-dar

Kikosi cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha cha Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam juzi katika tukio la majibizano ya risasi baina ya majambazi na polisi maeneo ya Mbezi kwa Yusuph Makondeni kiliwauwa watu 6 waliotuhumiwa kuwa majambazi.

Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam DCP, Lucas Mkondya wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema kabla ya tukio hilo kutokea, polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha kimejipanga kufanya tukio la ujambazi wa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa akitoka benki ya DTB tawi la Nyerere road na kwamba angepita katika barabara hiyo waliyokuwepo majambazi hao.
Amesema baada ya polisi kupata taarifa hiyo, waliwawekea mtego majambazi hao, na kubaini kuwa walikuwa wanalifukuza gari la mfanyabiashara huyo.
Ameeleza kuwa, baada ya majambazi kugundua wameingia katika mtego wa polisi walianza kufyatua risasi ndipo polisi nao wakajibu mashambulizi.
Amesema miili ya majambazi hao iko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio lingine, DCP Mkondya amesema Terehe 17, 9, 2016 maeneo ya Tegeta Masaiti majambazi watatu wakiwa na silaha walivamia duka la Abdallah Juma na kupora fedha za mauzo. Na kwamba polisi baada ya kupata taarifa waliwafukuza majambazi hao hata hivyo wananchi wenye hasira kali waliwakimbiza na kumuua jambazi mmoja huku waliobaki walifanikiwa kukimbia.