Uamuzi wa DC Kilombero kwa watendaji watakaobainika kuruhusu ndoa za utotoni
Mkuu
wa Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro, James Ihunyo amewaagiza
Wakurugenzi kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wa Vijiji, Kata na
Mitaa watakaothibitika kuwa na ndoa za utotoni katika maeneo yao ikiwa
ni njia mojawapo ya kutokomeza tatizo hilo.
Agizo
hilo limetolewa leo na Mkuu wa Wilaya hiyo alipokuwa akisoma hotuba
wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyoandaliwa na
Shirika la Plan International na kufanyika katika Kijiji cha Ihenga,
Mkoani humo.
Ihunyo
amesema kuwa pamoja na Mkakati wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya mwaka
2030 kuwa na lengo la usawa wa kijinsia na kuhakikisha haimuachi
msichana nyuma katika suala zima la maendeleo lakini kama hakutokuwa na
ufuatiliaji na utoaji wa taarifa juu ya changamoto za wasichana mikakati
hiyo haitafanikiwa.
“Ili
kuhakikisha tunakomesha ndoa za utotoni na kuhakikisha tunafikia
malengo ya Sera ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030, nawaagiza
wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili kuwachukulia hatua za kinidhamu
watendaji wote wa wilaya hii ambao watathibitika kuwa na wasichana
walioolewa chini ya umri wa miaka 18 katika maeneo hayo”, alisema
Ihunyo.
Pia,
amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha
kuwa wale wote wanaowaoa au kuwaoza wasichana chini ya umri wa miaka 18
wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Aidha,
amewaasa wasichana kujiepusha na mazingira hatarishi yanayowapelekea
kupata mimba au kuolewa kabla ya umri wao na kuwasisitiza kutoa taarifa
hata kwa siri kwenye ofisi za Serikali ili hatua stahiki za kisheria
zichukuliwe.
“Ndugu
wananchi, tatizo la kunyanyasa na kuwabagua wasichana bado ni kubwa
duniani, kutokana na utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) linasema kuwa katika kila
dakika 10 mahali fulani hapa duniani msichana anafariki kutokana na
ukandamizaji hivyo,ushirikiano wa hali ya juu unatakiwa kutoka kwa
Serikali, Mashirika, wazazi pamoja na watoto wa kike wenyewe”, aliongeza
Ihunyo.