Kuelekea uchumi wa viwanda nchini, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetakiwa kuboresha huduma sambamba na kufikia wakulima wengi kwa kuwapa mikopo ili kuinua sekta ya kilimo ambayo ndiyo mtoaji wa malighafi zinazotumiwa na viwanda hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Bodi ya pili ya TADB, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji ameitaka benki hiyo kupunguza gharama za riba ili kutoa fursa kwa wakulima wote hususani wadogo kumudu mikopo hiyo.
“Tunafahamu changamoto zilizopo sababu si rahisi kwa benki kuwekeza katika sekta ya kilimo, bodi iliyozinduliwa leo ni mboni ya wakulima na taifa letu, serikali inaitegemea benki hii ili kutekeleza mpango wake wa kuifanya Tanzania ya viwanda,” amesema na kuongeza
“TADB ina jukumu la kuboresha na kuinua sekta ya kilimo ili mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa uongezeke kutoka asilimia 28 iliyopo sasa pia iendelee kutoa fursa za ajira,” alisema Dk. Kijaji
dk-ashatu-kijajiNaibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji
Ameitaka bodi ya benki hiyo kuzingatia misingi ya utawala bora pamoja na kukwepa matumizi yasiyo na lazima ili ijiendeshe kwa faida.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TADB Rosebudi Kulijira, amesema ukosefu wa mtaji wa kutosha ni miongoni mwa changamoto zinazoipelekea benki hiyo kutofikia wakulima wengi nchini.
Ametaja changamoto nyengine kuwa ni mfumo mbovu wa ukopeshaji.
“Ombi letu kwa serikeli ituwezeshe kwa kutuongezea mtaji sababu dhamira yetu ni kupanua wigo wa utoaji hiduma zetu kwa kuwafikia wakulima wengi katika mikoa yote nchini,” amesema. Licha ya kuiomba serikali kuiwezesha benki hiyo kwa kuipa mtaji, Kulijira ameitaka serikali kuisaidia benki hiyo wakati inapotafuta mtaji katika benki na taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi.
Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru, ameitaka benki ya TADB kutimiza wajibu wake kisera ili kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kama sekta nyengine na kutoa ajira kwa watanzania wengi.
Bodi ya kwanza ya TADB iliteuliwa mwaka 2013 ambapo katika kipindi cha miaka mitatu imetoa mikopo yenye thamani ya sh. Bilioni 4 kwa wakulima wadogo zaidi ya 2000.