PIKIPIKI ILIYOTELEKEZWA KWA ZAIDI YA MWAKA MMOJA YAENDELEA KUZUA BALAA.
Mwananchi akipita kwa kuikwepa pikipiki
yenye namba za usajili T 684 CJZ aina ya Fokon iliyotelekezwa kwa zaidi
ya mwaka mmoja katika kituo cha waendesha bodaboda cha Maganga
Veterinary Jijini Dar es Salaam.
Mwonekano wa pikipiki hiyo kwa nyuma.
Pikipiki hiyo ikiwa katika kijiwe hicho cha Veterinary Maganga Temeke jijini Dar es Salaam.
PIKIPIKI yenye namba za usajili T 684
CJZ aina ya Fokon iliyotelekezwa kwa zaidi ya mwaka mmoja katika kituo
cha waendesha bodaboda cha Maganga Veterinary Temeke jijini Dar es
Salaam inazua hofu kwa wananchi na hata kwa askari polisi ambao
wameshindwa kuipeleka kituoni.
Imeelezwa kwamba pikipiki hiyo
iliegeshwa katika eneo hilo na mtu mmoja ambaye alifika nayo akiwa
akiiendesha mwishoni mwa mwaka jana.
Mmoja wa waendesha bodaboda wa kituo
hicho ambaye hakupenda kujitambulisha jina lake alisema pikipiki hiyo
inawapa hofu wananchi wa eneo hilo na hata waendesha bodaboda.
"Hata sisi wenyewe tuna hofu na
pikipiki hii ndio maana tunaegesha mbalimbali na pikipiki zetu na ndio
maana sitaki kutaja jina langu" alisema mwendesha bodaboda huyo.
Aliongeza kuwa awali baada ya
pikipiki hiyo kutelekezwa katika kituo hicho mtu yeyote alipokuwa
akiisogelea au kuigusa ilikuwa ikijiwasha yenyewe lakini baada ya kupita
mwezi mmoja iliacha kujiwasha jambo ambalo limeongeza hofu kwa
wananchi.
Mkazi mwingine wa eneo hilo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Ismail alisema hata walipotoa taarifa
kituo cha polisi cha Maganga walishindwa kuichukua pikipiki hiyo
kutokana na tabia ya kujiwasha.
Alisema aaskari wa kituo hicho
ambacho kipo mita 10 na eneo ambalo ipo pikipiki hiyo walitoa taarifa
kwa wenzao wa kituo cha Chang'ombe ambao nao wameshindwa kuichukua na
kwenda nayo kituoni kwa ajili ya kumtambua mmiliki wa pikipiki hiyo
kupitia namba zake za usajili.
Ismail alisema inawezekana pikipiki
hiyo ilifungwa kifaa maalumu cha utambuzi iwapo kama imeibiwa na ndio
maana ilipokuwa ikiguswa au kusogelewa inajiwasha yenyewe licha ya
baadhi ya watu wanahusisha kujiwasha kwake na imani za ushirikina.
Imeelezwa kuwa pikipiki hiyo wakati
inatelekezwa ilikuwa katika hali ya upya lakini hivi sasa imeanza
kupoteza upya wake kwa kukosa huduma ya matunzo.
Jitihada za mtandao huu kumpata
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo wa Maganga ili kuzungumzia suala hilo
zimeshindika baada ya kuelekezwa alikuwa Manispaa ya Temeke kwenye
mkutano.