BOMOA BOMOA JIJINI DAR ES SALAAM, WENGI WALIA NA ZOEZI HILO.
Mkazi wa eneo hilo, Lukia Khalid (aliye kaa), akiwa amekaa nje na vyombo vyake baada ya kubolewa nyumba yake.
Wananchi wa Tegeta A Kata ya Goba
wakiwa wamesimama chini ya mti Dar es Salaam jana, baada ya nyumba zao
kubomolewa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa madai ya kuvamia eneo hilo.
Hata hivyo wamekanusha kuvamia eneo hilo. Zaidi ya nyumba 150
zilibomolewa. Wananchi hao leo wanaandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya
Ubungo kupeleka malalamiko yao.
Askari polisi wakiwa eneo hilo kuimarisha ulinzi.
Watoto wakiangalia nyumba yao baada ya kubomolewa.
Mkazi wa eneo hilo akiwa kando ya nyumba yake iliyobomolewa.
Mkazi wa eneo hilo akiangalia nyumba yake baada ya kubomolewa.
Magodoro yakiwa yamefunikwa na paa la nyumba baada ya kubomolewa kwa nyumba hizo.
KAMPUNI ya
Udali ya Yono Aution Mart imebomoa nyumba zaidi ya 150 za wakazi wa
Tegeta A Kata ya Goba jijini Dar es Salaam kwa madai ya kujengwa eneo
ambalo sio lao huku Kaya zaidi ya 450 zikikosa makazi ya kuishi.
Hata hivyo ubomojai huo umepingwa na wananchi hao wakidai eneo hilo ni lao na wapo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Zoezi la
ubomoaji wa nyumba hizo lililofanyika Dar es Salaam jana, ulisimamiwa na
askari polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi huku
wakiwa katika magari yenye namba PT, 3475, 1986 na 3675 huko kukiwa na
askari hao zaidi ya 15.
Mmoja wa
wananchi hao, Macarios Turuka akizungumza na Jambo Leo eneo la tukio
alisema eneo hilo kwa kipindi kirefu lilikuwa halitumiki na lilikuwa ni
vichaka vya wahalifu kwani wanawake walikuwa wakibakwa na kutumiwa na
watu kwa uhalifu ndipo walipoingia na kujenga.
Aliongeza kuwa
baada ya kuanza ujenzi ndipo alipo ibuka Benjamini Mutabagwa na kueleza
kuwa ni lake ndipo walipofungua kesi mahakama ya Kimara ambapo
alishindwa kupeleka vielelezo vya umiliki wa eneo hilo.
Mwanasheria
anayewatetea wananchi hao, Moses Chunga alisema kitengo cha kubomoa
nyumba hizo ni kukiuka sheria za mahakama kwani kuna kesi ya msingi
namba 188/ 2016 waliyofungua mahakama kuu ya ardhi ambapo walitakiwa
tarehe 31 mwezi huu kwenda kuisikiliza lakini wanashangaa kuona nyumba
hizo zikibomolewa.
Alisema
wananchi hao wanajipanga kudai fidia ya uhalibifu huo na kuwa kabla ya
yote wanahitaji kumuona rais kuona wanapata haki yao.
Mkurugenzi wa
Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, Yono Kevela alisema kampuni ya
ke imevunja nyumba hizo kwa amri ya mahakama na polisi walikuwepo
kusimamia zoezi hilo.
"Mwenye eneo
hilo ambaye ni Kanisa la Winers alishinda kesi mwaka mmoja uliopita na
leo jana ulikuwa ni utekelezaji wa kuwaondoa wavamizi hao" alisema
Kevela.
Mkazi wa eneo
hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamisi alisema kitendo
walichofanyiwa si cha uungwana hata kidogo kwani wao wapo katika eneo
kwa siku nyingi mpaka wamefikia hatua ya kujenga nyumba hizo hizo
mmiliki huyo alikuwa wapi kwa siku zote hizo.
"Kwa kweli hawa watu wanatufanya tusiipende serikali yetu tunaomuomba rais atusaidie katika jambo hili" alisema Hamisi.
Hamisi alisema
kesho leo wanatarajia kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Ubungo kupeleka kilio
chao na kama akishindwa watakwenda kwa mkuu wa mkoa na kama napo
hawatapata ufumbuzi watakwenda kumuona waziri Lukuvi na Rais.
Hawa Musa alisema baada ya kuvunjiwa nyumba zao wapo katika wakati mgumu na hawajui wataisheje na watoto wao.
Alisema
wamepanga vitu vyao nje na mvua yote iliyonyesha jana imelowanisha
vyombo vyao yakiwemo magodoro na hawajui huyo mtu anayedai ni eneo lake
nyuma yake yupo nani.
Alisema nyumba yake iliyobomolewa ilikuwa inathamani ya sh. 700,000.
"Tangua
tufungue kesi mahakama ya Kimara hakuwahi kufika kama yupo kweli kwanini
anashindwa kuhudhuria mahakamani " alihoji Musa.
Musa aliongeza
kuwa kabla ya kubomoa nyumba hizo walipaswa kutoa notsi lakini wao
hawajafanya hivyo wamefika saa mbili asubuhi na kuanza kubomoa bila hata
ya kuwa shirikisha vipongozi wa eneo hilo.
Mkazi mwingine
wa eneo hilo Juma Abdallah amelalamikia jeshi la polisi kwa kuchukua TV,
king'amuzi na sh. 80,000 zilizokuwepo ndani kabla ya nyumba yake
kubomolewa.
"TV yangu na king'amuzi na sh.80,000 zimechukuliwa wakati wa zoezi hilo" alisema Abdallah.
Katika hatua
nyingine wananchi hao wamemtupia lawama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa
wa Tegeta A kuwa amekuwa akiwakumbatia watu wanaodai kuwa eneo hilo ni
lao wakati anaelewa fika ukweli halisi wa eneo hilo.
Mwenyekiti huyo
Marko Vaginga alipopigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari
kuzungumza chochote zaidi ya kumtaka mwandishi kwenda ofisini kwake kwa
mazungumzo zaidi.
"Nakuomba uje ofisini tuzungumze kwa leo sipo tayari kuzungumza chochote" alisema Vaginga na kukata simu.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alipopigiwa simu alisema polisi
walikuwa eneo hilo kwa ajili ya kusimamia amri ya mahakama.