makerere-at-90-mwalimu-julius-kambarage-nyerere-3

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshauriwa kutokubali kushirikiana na serikali ya Morocco hadi itakapo kubali kuiacha huru nchi ya Sahara Magharibi, kwa kuwa isipo fanya hivyo Tanzania itakuwa inakiuka misingi ya mwasisi wa Taifa Mwl. Julias Kambarage Nyerere aliyepinga nchi za Afrika kutaliwa.

Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi (TASSC). Kamati hiyo pia imepinga ujio wa Mfalme wa nchi ya Morocco Mohamed wa Sita ambapo atafanya ziara ya siku 2 kuanzia Oktoba 23 hadi 25 mwaka huu.
Kamati hiyo imeeleza kuwa, nchi ya Moroko inaitawala Sahara Magharibi kwa kipindi cha miongo minne mfululizo kinyume cha taratibu na sheria za kimataifa.
Mratibu wa Haki za Binadamu TASSC Alphonce Lusako amesema kamati hiyo inasikitishwa sana na kitendo cha Moroccoo kuendelea kuikalia kimabavu nchi ya Sahara Magharibi licha ya uamuzi wa kihistoria uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya haki (ICJ) kwenye hukumu yake ya 1975 kwamba hakuna mausiano yoyote ya kihistoria au ya kisheria baina ya Sahara Magharibi na Morocco yanayoweza kuinyima nchi ya Sahara haki yake ya kujitawala.
“Tunamtaka rais wa Morocco kuacha mara moja kunyonya rasilimali za Sahara Magharibi hasa madini ya Fosfeti na rasilimali bahari katika eneo inayokalia kimabavu,” amesema.
Amesema kuwa, serikali ya Tanzania isitoe ushirikiano kwa Rais wa Morocco hadi atakapo kubali kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na wanaharakati wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali kwenye maeneo ya Sahara Magharibi.
Mratibu wa Mawasiliano kwa Umma Noel Shao ametoa wito kwa Umoja wa Afrika kutoikubalia Moroko kurejea kwenye umoja huo hadi itakapoacha kuikalia kimabavu Sahara ya Magharibi.
Shao pia ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuharakisha mchakato wa kura ya maoni ya kuipatia Sahara Magharibi uhuru wake.