WANAFUNZI 22,000 WAJENGEWA UWEZO WA KUJIAMINI GRUMETI FUND
wanafunzi wa kike 22,000 wamejengewa uwezo wakujiamini kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwepo vitendo vya ukatili wa kijinsia ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikisababisha washindwe kufikia ndoto zao za kielimu.
Wanafunzi hao ni wa kutoka katika shule zinazozunguka mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo katika wilaya za Bunda na Serengeti mkoani Mara.
Ofisa Elimu wa Grumeti Fund, Elizabeth Magoto amesema elimu hiyo imetolewa na shirika lake kupitia makongamano yanayoshirikisha wanafunzi kutoka katika shule hizo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambapo takriban makongamano 90 yamefanyika.
Akizungumza katika kongamano la kujadili changamoto hizo Julai 20,2026 liloandaliwa na shirika hilo na kufanyika katika shule ya Sekondari Natta wilayani Serengeti, Elizabeth amesema makongamano hayo tayari yamekuwa na matokeo chanya.
" Tumekuwa na utaratibu wa kuandaa makongamano ya aina hii ili kuwawezesha wanafunzi wa kike kujadili changamoto sambamba na kupata mbinu za kukabiliana nazo na tayari matokeo chanya yameanza kuonekana," amesema
Amesema matokeo hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watoto wa kike wanaoomba ufadhili wa masomo ya ngazi za juu kutoka katika shirika hilo ambapo ongezeko hilo limehusisha pia wanafunzi wa kike wanaoomba ufadhili kwaajili ya masomo ya sayansi.
"Kwasasa tuna uwiano wa maombi ya 50/50 kwa wanafunzi wa kike na wa kiume tena hapo kuna ongezeko la wanafunzi wa kike wanaoomba ufadhili wa masomo ya sayansi tofauti na zamani ambapo kulikuwa na uwiano wa 30/70 ambapo wanafunzi wa kike walikuwa wanaomba ufadhili kwa masomo ya sanaa" amesema
Meneja Rasilimali Watu wa Shirika la Grumeti Fund, Amsi Nyambuche amesema shurika hilo litaendela kufanya makongamano ya namna hiyo ili kuendelea kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike kukabiliana na changamoto zinazowakabili na hatimaye waweze kufikia malengo yao.
Amesema katika makongamano hayo wanafunzi hao pamoja na kujadili changamoto hizo pia wamekuwa wakipata fursa ya kukutana na watu mbalimbali ili kupata uzoefu wao kwa namna walivyoweza kupambana na vikwazo na hatimaye kufikia malengo waliyokusudia.
"Wasichana kutoka katika jamii hii bado wanakumbana na changamoto nyingi hivyo tumeamua kuangalia namna gani tunaweza kuwawezesha kujikwamua na kufikia ndoto hasa za elimu kama tunavyojua elimu ndio msingi wa maisha," amesema.
Wakizungumza katika kongamano hilo, baadhi ya wanafunzi wamesema zipo changamoto kadhaa ambazo wanakumbana nazo hali ambayo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ni kikwazo kwa watoto wa kike kufikia malengo yao.
Changamoto hizo ni pamoja na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni hali inayosababisha wakose baadahi ya vipindi sambamba na kukosa muda wa kujisomea kutokana na kutakiwa kufanya kazi za nyumbani hivyo kuomba kujengwa kwa hosteli kwaajili ya watoto wa kike katika shule zote za sekondari ili waweze kundokana na changamoto hizo.
Magori Kaitira amesema jamii inapaswa kubadilika na kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zikiwakandamiza watoto wa kike na kwamba badala yake watoto hao wapewe haki sawa kwaaili ya ustawi wa jamii nzima.
Amesema dhana ya kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi katika jamii imepitwa na wakati kwa maelezo kuwa ipo mifano hai ya viongozi kuanzia ngazi za vitongoji hadi kitaifa na kimataifa ambao wamepata fursa za kuwa viongozi na kufanya kazi zao kwa weledi hivyo jamii inapaswa kuwaunga mkono watoto wa kike ili kuweza kupata viongozi bora bila kujali jinsia.
Fatuma Ramadhani amesema umefika wakati sasa Serikali pamoja na wadau wa haki za binadamu kuangalia njia mbadala ili kumaliza changamoto hiyo ambayo imekuwa kikwazo cha maendeleo kwa wasichana wengi katika jamii.
Amesema jamii inapaswa
kubadilika na kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati ambazo
zimekuwa zikiwakandamiza watoto wa kike na kwamba badala yake watoto hao
wapewe haki sawa kwaaili ya ustawi wa
jamii nzima.