WANANCHI MARA WAMEACHANA NA KILIMO CHA BANG-RC MARAI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amempokea na kuzungumza na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Ndugu Aretas James Lyimo ambapo amesema kuwa kuna mabadiliko makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa za maendeleo zilizopo na kuachana na kilimo na biashara ya dawa za kulevya.
“Kwa sasa wananchi wanajishughulisha zaidi na shughuli za kuwaletea maendeleo endelevu ikiwemo uchimbaji wa madini, uvuvi, ufugaji wa samamki kwenye vizimba, kilimo na shughuli nyingine halali na hawahangaiki tena na kilimo cha bangi kama ilivyokuwa hapo awali” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema wananchi wengi wameendelea kubadilika kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wananchi katika kupambana na kilimo, biashara na matumizi ya dawa za kulevya hususan bangi.
Kanali Mtambi amesema baada ya kudhibiti kilimo na biashara za dawa za kulevya matukio ya uhalifu katika Mkoa wa Mara kwa sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa na kuongeza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wananchi.
Kwa upande wake, Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Ndugu Aretas James Lyimo amesema mafanikio yaliyopatikana katika Mkoa wa Mara yanadhihirisha ushirikiano mzuri uliopo baina ya Mamlaka hiyo, viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika tukio hilo, Ndugu Lyimo amesema kwa sasa takribani asilimia 80 ya wananchi wa Mkoa wa Mara wameachana na kilimo na biashara ya bangi kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya DCEA, viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Hapo zamani ilikuwa ni jambo la kawaida kukuta mashamba ya mahindi au mazao mengine yakiwa na bangi katika Mkoa wa Mara lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa sana” amesema Ndugu Lyimo.
Ndugu Lyimo ameshukuru ushirikiano unaoendelea kutolewa kwa Mamlaka hiyo na viongozi wa Mkoa wa Mara katika operesheni mbalimbali za kudhibiti dawa za kulevya zinazofanyika katika Mkoa huo jambo ambalo amesema limesaidia kupungua athari za madawa hayo kwa maendeleo ya Taifa na hususan kwa nguvukazi ya vijana na usalama wa rasilimali za nchi.
Ndugu Lyimo amesema baadhi ya mataifa au makundi yenye maslahi hasi yanaweza kutumia dawa za kulevya kama njia ya kudhoofisha nguvu kazi ya taifa na kupunguza uzalishaji na kuongeza kuwa kama vijana wengi watakuwa wameathirika na dawa za kulevya inaweza kuhatarisha maendeleo na usalama wa Taifa.
