WANANCHI WATAKIWA KUJIHEPUSHA NA MATUKIO YA MAUAJI .
Yamesemwa hayo Julai 22, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi wa Kata hiyo kupitia kampeni ya Serikali Nyumbani Kwako, inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu.
Vilevile, Kamanda Senga alisema kuwa matukio mengi ya mauaji yanayotokea katika jamii husababishwa na migogoro ya kifamilia, wivu wa kimapenzi, imani potofu za kishirikina pamoja na wananchi kujichukulia sheria mkononi badala ya kufuata taratibu za kisheria, aliwataka wananchi hao kuachana na tabia hizo na kutumia njia za mazungumzo pamoja na vyombo husika kutatua migogoro
Kamanda Senga aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe ikiwa ni pamoja na Polisi Kata na viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mapema kabla ya madhara kutokea.
Aidha Senga alisisitiza kuwa ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi na kwamba hakuna mtu anayepaswa kujichukulia sheria mkononi, huku akiongeza kuwa jamii yenye mshikamano na ushirikiano ndiyo msingi wa kudumisha amani na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
