NDEJEMBI AAGIZA MRADI UKAMILIKE HARAKA



Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi zilizobaki za mradi wa njia ya umeme wa kilovoti 33 (KV 33) kutoka Masasi hadi Newala kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika.


Aidha, Waziri Ndejembi amempa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) muda wa wiki tatu kuhakikisha huduma ya umeme inaunganishwa pia katika Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara.

Maagizo hayo ameyatoa wakati wa uzinduzi wa njia ya umeme ya KV 33 kutoka Masasi hadi Newala yenye thamani ya shilingi bilioni 4.65, mradi unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme na kumaliza changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa umeme katika Wilaya ya Newala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msangi, amesema uwekezaji huo utafungua fursa za uwekezaji, biashara na maendeleo ya kijamii katika mkoa huo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Razaro Twange, amesema mradi huo utapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la kukatika kwa umeme, kuboresha upatikanaji wa huduma na kuchochea shughuli za maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yanayohudumiwa.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Newala wameeleza matumaini yao kuwa mradi huo utamaliza changamoto ya kukatika kwa umeme na kurahisisha shughuli za biashara, uzalishaji na huduma nyingine za kijamii.

Powered by Blogger.