RC MARA AZITAKA HALMASHAURI KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoa wa Mara kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati ili kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi.
 
 
Mhe. Mtambi amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mkoa wa Mara uliidhinishiwa bajeti ya matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo shilingi bilioni 400.17 na fedha hizo Serikali imeshazitoa hadi kufikia mwezi Oktoba, 2025 lakini kasi ya Halmashauri kutekeleza miradi hiyo hairidhishi. 
 
“Mimi siridhishwi na kasi ya utekelezaji wa miradi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa niwatake Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha fedha zote zilizopokelewa zinatumika na kukamilisha shughuli zilizopangwa kabla ya Juni, 2026” amesema Mhe. Mtambi. 
 
Mhe. Mtambi amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri zilivuka na kiasi cha shilingi bilioni 26.96 iliyopangwa kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa mwaka huo na hadi Disemba, 2025 asilimia 28 ya fedha hizo bado zilikuwa hazijatumika na ametoa hadi mwishoni mwa Machi, 2026 miradi yote ya 2024/2025 iwe imekamilika. 
 
Kanali Mtambi amesema Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo hadi Disemba, 2025 zilikuwa hazijatumika na amewataka Wabunge wa Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa vikao vya Kamati ya Mfuko wa Jimbo vinakaa na kupeleka fedha hizo katika utekelezaji wa miradi. 
 
Mhe. Mtambi amesema kwa mujibu wa kifungo cha (xi) katika Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati 2026/27-2028/29, kuwa mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali haitaruhusu kuvuka na fedha ifikapo mwisho wa mwaka na kuzitaka Halmashauri kukamilisha miradi yao kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha. 
 
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mara kuongeza juhudi katika kuboresha makusanyo ya mapato ya ndani yaliyotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ili kuboresha huduma kwa wnaanchi. 
“Mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri zetu hauridhishi na hadi mwezi Disemba, 2025 Halmashauri zilikuwa zimekusanya shilingi bilioni 23.76 tu kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 51.50 kwa mwaka 2025/2026” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri kusimamia vyanzo vyote vya mapato kikamilifu pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kupeleka fedha zitakazopatikana katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya
Mhe. Mtambi amezipongeza Halmashauri kwa kupeleka fedha za mapato ya ndnai katika miradi ya maendeleo na kuzipongeza Halmashauri za Bunda DC na Bunda TC ambazo zimepeleka zaidi ya asilimia 100 ya kiasi kilichotakiwa kupeleka.
Kwa upande wake akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Ndugu Iddi Mkoa amezitaka Halmashauri kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati.
Ndugu Mkoa pia amewapongeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Watendaji wa Taasisi za umma kwa namna wanavyotoa ushirikiano, kutekeleza majukumu yao na wamekuwa wasikivu na wanaoshaurika katika kuboresha utendajikazi wa taasisi zao.
Kikao cha RCC kimehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Meya, Wenyeviti na wataalamu wa Halmashauri, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa maendeleo.
Powered by Blogger.