WAJASILIAMALI WA SALUNI MANISPAA YA MUSOMA WANAUME NA WANAWAKE WAPEWA VIFAA VYAKAZI

 

Wajasiriamali wadogo wa saluni za kike na kiume zaidi ya 60 wamepewa vifaa vya kazi kwaajili ya kuboresha shughuli zao huku wakitakiwa kurasimisha biashara ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea endapo shughuli hizo hazitarasimishwa.

Msaada huo wa vifaa ni pamoja na mashine za kukaushia nywele, mashine za kunyolea, majaketi pamoja na sabuni na spiriti vifaa ambavyo vimetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Marwa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo mjini Musoma leo Jumanne Machi 3,2026 mbunge huyo amesema ametoa vifaa hivyo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha shughuli za wananchi hususan wale wa makundi yasiyokuwa rasmi.

Amesema wafanyabiashara wasio rasmi wana mchango mkubwa katika uchumi wa kaya, jamii na taifa kwa ujumla hivyo ipo haja ya wadau mbali kuungana na Serikali katika kuwasaidia ili waweze kuboresha shughuli zao.

"Mimi mwenyewe nimetokea huku,nilikuwa muuza dagaa nimeuza   mahindi hivyo najua changamoto za sekta hii na nimeamua kuwa nitawafikia wote, kwa leo nimeamua kutumia sehemu ya mshahara wangu wa Februari ili kusaidia kuboresha shughuli zao," amesema 


Amesema msaada huo hauna itikadi ya chama chochote cha siasa  isipokuwa anautoa kwa lengo la kuboresha shughuli za wajasirimalia hao kwa maelezo kuwa maendeleo hayana chama cha siasa bali ni suala la jamii nzima.

Mbunge huyo amefafanua kuwa licha ya uwepo wa fursa za mikopo isiyokuwa riba bado wapo baadhi ya wajasiriamali  ambao wanashindwa kupata mikopo hiyo kutokana na sababu mbalimbali ndani ya jamii hivyo ameona hakuna haja ya kundi hilo kuachwa nyuma katika safari ya maendeleo.

"Rais Samia tayari amesema anataka kuacha tabasamu kwa wananchi,sisi tunapaswa kumuunga mkono tunapaswa kuangalia makundi yapi yanahitaji nini ili tuwe sehemu ya kuacha tabasamu kwa wananchi kwa kushirikiana na Rais wetu,kwangu mimi huu ni mwanzo tu nitajitajidi kuyafikia makundi yote," amesema.


Akizungumza na wajasiriamali hao, Ofisa Biashara wa Manispaa ya Musoma, Charles Sayungu amewataka kuhakikisha wanarasimisha shughuli zao ili waweze kutambuliwa na kuunganishwa na fursa mbalimbali.



Amesema urasimishaji wa shughuli zao unahusisha kukata leseni sambamba na kulipa ada ya Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

"Kwa shilingi 40,000 unapata leseni yako huku ada ya Basata ikiwa ni shilingi 20,000 tu hivyo kwa mwaka mzima unatakiwa kulipa jumla ya shilingi 60,000," amesema 

Amesema miongoni mwa madhara yanayoweza kuwapata endapo hawatarasimisha  biashara zao ni pamoja na kufungiwa shughuli zao pamoja na kukosa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo kutoka taasisi za kifedha.


Mkuu wa Wilaya ya Musoma,Juma Chikoka amemshukuru mbunge huyo kwa msaada huo ambao amesema utasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha shughuli za walengwa na maisha yao kwa ujumla.

















Powered by Blogger.