WATANO MBARONI KWA TUHUMA ZA KUIBA KWENYE DALADALA MWANZA

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za wizi ndani ya usafiri wa umma aina ya daladala katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyamagana na Ilemela.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa waandishi wa habari  na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya uwepo wa vitendo hivyo vya kihalifu kwenye vyombo vya usafiri.

"Watuhumiwa hao wamekamatwa wakati wa oparesheni iliyoanza Tarehe 19.01.2026 hadi 
31.01.2026 kufuatia taarifa za malalamiko zilizopokelewa na Jeshi la Polisi kutoka kwa 
wananchi juu ya uwepo wa vitendo hivyo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la 
Mwanza," amesema

Sambamba na hilo Kamanda Mutafungwa amesema pia Jeshi hilo linawashikiria madereva tisa pamoja na makondakta watano kwa tuhuma za  kukatisha njia na kutofika sehemu husika iliyoainishwa kwenye leseni zao za usafirishaji.

"Watuhumiwa 9 ni madereva na 5 ni makondakta ambao nao wanashikiliwa kwa kosa la kukatisha njia na kutofika sehemu husika iliyoainishwa kwenye leseni zao za usafirishaji, pamoja na magari 13  ambayo yamehusika katika uhalifu huo," amesema Kamanda Mutafungwa



Powered by Blogger.