BENKI YA NMB YATENGA BILIONI 7.4 KUSAIDIA MIRADI YA KIJAMII

 






Benki ya NMB inatarajia kutumia zaidi ya Sh7.4 bilioni kwaajili ya kusaidia miradi mbalimbali katika jamii nchini hususani kwenye sekta za elimu, afya na mazingira kwa mwaka 2026 ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa benki hiyo kurudisha shukrani kwa jamii.

Kiasi hicho cha fedha kimetengwa baada ya  benki hiyo kupata faida ya zaidi ya
Sh746 bilioni ambayo benki hiyo ilipata kwa mwaka 2025.

Takwimu hizo zimetolewa wilayani Rorya leo Jumamosi Januari 31,2026 na Mkurugenzi wa Fedha NMB, Juma Kimori alipokuwa akikabidhi vifaa kwaajili ya kuimarisha sekta za afya na elimu mkoani Mara vifaa vilivyo gharimu zaidi ya Sh430 milioni.

Kimori amesema benki hiyo inatambua jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za jamii hasa katika sekta hizo za afya,elimu na mazingira hivyo kutokana na umuhimu wa sekta hizo benki hiyo imeamua kuunga mkono jitihada hizo ili huduma zitolewazo kupitia sekta hizo ziweze kuwa bora zaidi.


"Tuna akaunti zaidi ya milioni tisa ambazo zinatokana na wana jamii hawa hawa hivyo tumeona kuna haja ya kutoa shukrani kwao  kwa kutuchagua na tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii ili tuwe na jamii bora zaidi," 


Kimori ameeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita benki hiyo imetumia zaidi ya Sh23 bilioni kwaajili ya kuboresha huduma za kijamii katika sekta hizo huku benki hiyo ikiwezesha upandaji wa miti zaidi ya milioni moja kwa mwaka 2024/25 ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. 

Akizungumza kuhusu vifaa vilivyokabidhiwa leo,Kimori amesema vifaa hivyo ni pamoja na mashine nane kwaajili ya joto kwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda, magodoro, vitanda,mashuka, madawati na vifaa kwaajili ya kuezeka madarasa msaada ambao umetolewa kwa wilaya sita za mkoa wa Mara.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo huku akitoa wito kwa wana jamii wilayani humo kuwapeleka watoto wao shule kwa maelezo kuwa bado wapo wanafunzi wa madarasa ya awali,la kwanza na kidato cha kwanza hawajaripoti shuleni hadi sasa.

Dk Haule amesema msako wa kuwatafuta wazazi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni unatarajiwa kuanza wilayani humo kuanzia Februari 2 2026 ingawa hakuweza kutoa takwimu za wanafunzi ambao bado hawajaripoti shuleni.

Amesema Serikali wilayani humo tayari imetoa maelekezo kwa walimu kuwapokea wanafunzi wote hata kama hawana mahitaji ya msingi ikiwepo sare za shule,daftari na kalamu kwa maelezo kuwa tayari ofisi yake imefanya mchakato wa kuwawezesha wanafunzi wanaotoka kaya masikini kuweza kuanza masomo bila kikwazo.

"Jukumu la mtoto ni kusoma hili la mahitaji ya msingi ni jukumu la mzazi lakini ofisi yangu pia tayari imepata mabegi,madaftari kwaajili ya wale watoto wanaotoka kwenye kaya masikini ili kuwawezesha waanze masomo wakati wazazi wanaendelea kuwatafutia mahitaji hayo," amesema 


Akizungumza baada ya kupokea msaada wa mshine nane za joto kwaajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda,Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Shirati KMT, Dk Bwire Chirangi amesema hospitali hiyo bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mashine hizo.

Dk Bwire Chirangi amesema wastani wa akinamama 300 hujifungua hospitalini hapo kila mwezi ambapo kati ya hao, watoto 30 huzaliwa kabla ya muda hivyo kuhitaji huduma za ziada ili kuwawzesha kuishi ikiwemo mashine za joto.

Amesema baada ya kupokea msaada huo hospitali hiyo inakuwa na jumla ya mashine 10 kwaajili ya watoto hao idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda katika hospitali hiyo.

Amesema upungufu huo kwa namna moja ama nyingine unawapa wakati mgumunwao kama watoa huduma katika harakati zao za kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya umri.

 

Powered by Blogger.