RC MAKAME AIPONGEZA REA KUWAPELEKEA UMEME WATEJA 6,135 SONGWE
📌Vitongoji 173 kupelekewa umeme kwa bilioni 28.3
📌Mkandarasi atakiwa kutekeleza mradi kwa kasi
📍Songwe
Mkuu
wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Makame ameishukuru Serikali kupitia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni
28.3 kupeleka umeme kwa wateja 6,135 waliopo kwenye vitongoji 173
mkoani humo.
RC
Makame ametoa pongezi hizo leo Februari 2, 2026 mara baada ya kukutana
na Wataalam kutoka REA waliofika kumtambulisha mkandarasi wa mradi wa
HEP 2B kampuni ya M/s Jaitech Company Ltd atakayetekeleza mradi wa
kupeleka umeme vitongojini.
"Namshukuru sana
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kutuletea fedha hizi ili kupeleka umeme kwa wananchi wapatao 6,135
wa mkoa huu ili watumie nishati ya umeme," Amesema RC Makame.
Vilevile,
amemtaka mkandarasi wa mradi kutekeleza mradi huo kwa kasi na weledi
kwa kuwa wananchi wanamatumaini ya kuwashiwa umeme huo mapema ili
waendelee na shughuli za kiuchumi na kuwaletea maendeleo.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Bw. Frank Mugogo
ameeleza kuwa REA itaendelea kutekeleza miradi ya nishati ya umeme
vijijini kwa ubora na uhakika ili wananchi wapate umeme wa uhakika.
