WAKANDARASI WA KUSAMBAZA UMEME WATAKIWA KUONGEZA KASI
Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza miradi ya kusambaza
umeme vitongojini kwa lengo la kuhakikisha ifikapo Mwaka 2030 vitongoji
vyote viwe vimefikishiwa umeme.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya
Kusambaza Umeme REA, Mha. Deogratius Nagu ameyasema hayo Mkoani Ruvuma
Februari 1, 2026 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya kusambaza umeme
inayotekelezwa mkoani ili kujionea hali ya utekelezaji.
“Tupo
katika Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya
kusambaza umeme vitongojini inayotekelezwa na Wakala na leo hii tumefika
hapa Wilayani Mbinga kukagua mradi wa kupeleka umeme vitongoji 148
ujulikanao kama Mradi wa Ujazilizi Fungu 2C (Densification 2C)
unaohusisha Wilaya ya Songea, Mbinga na Nyasa,” amefafanua Mhandisi Nagu
Katika
ziara hiyo, Mha. Nagu amemuelekeza Mkandarasi anayetekeleza mradi,
kampuni ya MF Electrical Engineering Ltd kuhakikisha anaongeza kasi ya
ujenzi wa mradi ili akamilishe usambazaji wa umeme katika vitongoji 60
vilivyosalia katika mradi huo.
“Huu
mradi unahusisha usambazaji umeme katika vitongoji 148 ambapo vitongoji
88 tayari vimewashwa umeme na kubakiza vitongoji 60 ambavyo utekelezaji
unaendelea; tumemuelekeza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mapema
kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji alivyobakiza,” amesema Mha.
Nagu.
Akizungumza
kwa niaba ya Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi
Zakaria Ng’okorome amesema mradi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi
bilioni 18.294 na kwamba utanufaisha wateja wa awali wapatao 6,781.
Naye
Msimamizi wa Mradi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa
Ruvuma, Mha. Ali Pandit alisema wamejipanga kikamilifu kuhalkikisha
miradi inakamilika kwa wakati na kufikisha umeme kwa wananchi.


