HGWT YAIKUMBUSHA JAMII ULINZI DHIDI YA WATOTO WAKIKE.


JAMII imehimizwa kuendelea kuwalinda Watoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni pamoja na kuhakikisha wanapewa fursa ya elimu kikamilifu kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa Februari 6, 2026 Mjini Musoma na Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Mkoani Mara la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia Mkoani humo wakati akizungumza na Majira Online kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya ukeketaji ambayo kwa mwaka huu yatafanyika Februari 11, 2026 Wilayani Monduli Mkoani Arusha.

Amesema kuwa, Watoto wa kike Wana nafasi kubwa ya kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika jamii iwapo wakiwezeshwa kupata fursa ya elimu kama ilivyo kwa Watoto wa kiume. Jambo ambalo amesema kila mwanajamii anapaswa kuwajibika kulifanya.

Amehimiza jamii iachane na mila ambazo zimekuwa kikwazo kwa Watoto wa kike kutimiza ndoto zao ukiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na manyanyaso mengine ambayo huwarudisha nyuma katika harakati zao za kupiga hatua.

“Ukeketaji huchochea ndoa za utotoni, binti anapokeketwa anakuwa anaandaliwa aolewe haijalishi umri wake ni mdogo. Na kama anasoma basi, hawezi kuendelea na masomo tena. Niihimize jamii iungane na serikali na wadau wote kukemea ukeketaji, ndoa za utotoni na iweke mkazo katika kuwasomesha kwa juhudi zote.”amesema na kuongeza.

“Tunaishukuru sana serikali Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imebooresha mazingira ya watoto kusoma. Ili Watoto wote wasome bila ada na kuimarisha miundombinu mashuleni na pia walimu wameendelea kuajiriwa ili kila mtoto apate fursa ya elimu kwa faida yake, jamii na Taifa pia bila kisingizio chochote.”amesema Rhobi.

Aidha, Rhobi ameishukuru serikali kwa kuendelea kukemea vikali mila zisizofaa ambazo zimekuwa na madhara kwa Watoto wa kike na jamii, jambo ambalo amesema limeendelea kusaidia kwa kiwango kikubwa vitendo hivyo kuendelea kupungua. Huku akihimiza wadau wote kuendelea kushirikiana ili kuvitokomeza badala ya kuiachia serikali pekee jukumu hilo.

Beata Paulo ni Mkazi wa kata ya Mkendo Manisapaa ya Musoma ameiambia Majira Online kuwa, anafurahishwa kuona serikali ikiwachukulia hatua Kali za kisheria wanaobainika kufanya vitendo vya ukatili wa Kijinsia kwani kufanya hivyo ni kulinda usawa wa Kijinsia na ustawi bora unaoleta maendeleo katika jamii.

Rhoda Marwa mkazi wa Kata ya Bweri katika Manisapaa hiyo, amesema elimu iendelee kutolewa mashuleni, katika mikutano ya hadhara, kwa watu mashuhuri na makundi mbalimbali kuwezesha kutokomeza vitendo vya ukatili sio kwa jinsi ya kike pekee bali pia wanaume kwani wapo na huogopa kutoa taarifa katika vyombo vya kisheria.

“Tunao Viongozi wanawake katika nchi yetu ni Mawaziri, Wakuu wa Mkoa, na Rais wetu ni Mwanamke ambaye anafanya kazi vizuri kututumikia watanzania. Haya ni matunda ya elimu walisomeshwa kwa sasa Taifa wanalitumikia. Nitoe ushauri kwa jamii zinazokeketa watoto wa kike ziache. Ziwape fursa ya kusoma, pia wazazi waache tamaa ya mali hasa vijijini ng’ombe watano au saba wasimfanye mtoto wa kike ashindwe kuja kuwa Waziri kwa siku za usoni.”amesema Paulo Chacha.

Februari 11, 2026 ni kilele cha siku ya ukeketaji ambapo kwa mwaka huu itafanyika Wilayani Monduli Mkoani Arusha. Ambapo serikali na wadau wa masuala ya ukeketaji kujitathimini hatua iliyofikiwa katika kutekeleza afua za kutokomeza ukeketaji nchini ikiwemo mafanikio na changamoto na kubadilishana uzoefu na namna bora ya kukabiliana na ukeketaji unaofanywa na baadhi ya jamii hapa nchini.





 

Powered by Blogger.