BILIONI 91 KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI MORO

 

Serikali imedhamiria kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme Mkoani Morogoro kwa kutoa jumla ya shilingi bilioni 91 kwa ajili ya kusambaza umeme katika ngazi ya vitongoji. Hatua hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati wa mkutano na waandishi wa habari ambapo amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kila kitongoji kinapata umeme ili kuwawezesha wananchi kuongeza uzalishaji na vipato vyao.



Malima amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya umeme, akibainisha kuwa awali Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulipoanza kutekeleza miradi yake ulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 3 pekee, lakini kwa sasa Mkoa wa Morogoro umefanikiwa kupata shilingi bilioni 91 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Thomas Mmbaga, amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya vitongoji 3,391, ambapo hadi sasa umeme umesambazwa katika vitongoji 1,821. Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, vitongoji vyote vya mkoa huo vinakuwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

Naye Msimamizi wa Mradi, Kelvin Manaseh, amesema utekelezaji wa miradi hiyo utafanyika kwa wakati na kukamilika kama ilivyopangwa ili kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu.









Powered by Blogger.