NSSF Kuwaburuza Mahakamani WaaJiri 126


Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Arusha linatarajia kuwafikisha mahakamani waajiri 126 kwa kutowasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Dk. Frank Maduga amesema kuwa waajiri hao wameshindwa kuwasilisha michango hiyo kwa zaidi ya miezi sita ambayo ni zaidi ya Sh bilioni moja.

“Kati ya hao waajiri wakubwa ni 14, waajiri wa kati 69 na waajiri wadogo 53, ambapo wote walishapelekewa onyo la mwisho na taratibu za kuwafungulia mashitaka zimeshakamilika na wiki ijayo tunatarajia kuwafikisha mahakamani kwani kutokuwasilishwa kwa michango hiyo kumekuwa na madhara kwa wanachama na wategemezi wao."

Hata hivyo Dk. Maduga alikataa kutaja majina ya mashirika hayo ambapo amesema yatatajwa mahakamani wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaandaa hati za mashtaka.

Pamoja na mambo mengine, meneja huyo amesema kwa sasa shirika hilo limeingia mkataba na hospitali inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ya Selian, ambapo wanawake wajawazito ambao ni wanachama watapatiwa matibabu bure na kuwa wanatarajia kuingia mkataba na hospitali nyingine zaidi.
Powered by Blogger.