KAULI YA BANYAI KISA CHA KUACHANA NA NJOMBE MJI;

Kikosi cha Njombe Mji
SIWADAI hawanidai! hiyo ni kauli ya aliyekuwa kocha wa Njombe Mji Hassan Banyai baada ya kubwaga manyanga kuifundisha timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu.
Banyai amesema baada ya kuandika barua hiyo kwa Mwenyekiti wa klabu Erasto Mpete alimpatia stahiki zake zote ambapo kwa sasa yupo huru kujiunga na timu yoyote.
Kocha huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa moja ya sababu iliyomfanya kuachia ngazi ni msimamo wake ambapo kuna kipindi alikuwa akipangiwa kikosi kitu kilichofanya kukinzana na uongozi.
“Ukiacha kutishiwa maisha na mashabiki lakini pia msimamo wangu umeniondoa Njombe Mji. Ningeondoka kabla ya mechi ya pili dhidi ya Yanga lakini nikavumilia lakini yaliyotokea nimeamua kuachana nao kwa amani, mimi ni kocha mweledi mwenye misimamo, siwezi kupangiwa,” alisema Banyai.
Banyai alisema pia uongozi ulimtaka ajitathimini kama anapaswa kuendelea baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo lakini kabla ya hapo aliwaomba wamfanyie mambo sita ili timu ifanye vizuri kwenye ligi cha ajabu walifanikiwa jambo moja tu.
“Niliwambia mambo sita ambayo ni usajili, kambi nzuri, vifaa vya maandalizi, usafiri, uwanja wa mazoezi na mechi za majaribio. Katika mambo hayo walifanikiwa moja tu mechi za majaribio nilipata tano, sasa kati yangu mimi na wao nani anapaswa ajitathimini,” alihoji Banyai.
Wakati huo huo kocha huyo alisema muda mfupi tu baada ya kuachana na timu hiyo amepokea ofa tatu kutoka kwa timu zinazohitaji huduma yake.