Kakolanya ‘alia’ kuendelea kukaa nje;

MLINDA mlango wa timu ya Yanga Beno Kakolanya amebainisha kuwa kitendo cha kukaa nje ya uwanja muda mrefu kinamuumiza sana kwavile anapitwa na vitu vingi ikiwemo kushindwa kuwasaidia mabingwa hao katika mechi zake zinazoendelea.
Kipa huyo wa zamani Tanzania Prisons alipata majeraha ya nyonga akiwa kwenye maandalizi ya kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kilichokuwa kikijiandaa kwenda kushiriki michuano ya COSAFA iliyofanyika nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka huu.
Hata hivyo Kakolanya alicheza mechi moja ya kirafiki ya Yanga dhidi ya Singida United mwezi Agosti waliyoshinda mabao 3-2 na kuumia tena hali iliyopelekea akae nje uwanja hadi sasa.

Youthe Rostand amecheza mechi zote tatu za ligi akifungwa mabao mawili
Kakolanya ameiambia MAKALIBLOG. kuwa anaumia sana kukaq nje ya uwanja huku akifahamu ana uwezo wa kuisaidia timu yake kufanya vizuri kutokana na uzoefu alionao.
“Unajua unapokaa nje ya uwanja muda mrefu kuna vitu vinakupita, tayari timu imecheza mechi tatu za ligi mpaka sasa na sikuwepo katika maandalizi ya msimu huu kwahiyo naona nashindwa kuisaidia Yanga kutokana na majeraha,” alisema Kakolanya.
Kipa huyo alisema atafanya mazoezi sana ili kujiweka sawa kwa lengo la kuwafikia wenzake ambao amekiri wamemuacha mbali sana.