MTANZANIA AHUKUMIWA JELA MIEZI MITATU KWA KURUSHA 'Kupost' FACEBOOK PICHA YA MAREHEMU
Mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa ni
Mtanzania amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela nchini Uingereza kwa
kosa la kurusha katika ukurasa wake wa Facebook, picha za mtu
aliyefariki dunia kutokana na moto uliounguza jengo la ghorofa la Mnara
wa Grenfell lililopo nchini humo.
Pia, mtu huyo ametakiwa kulipa faini ya Sh579,880 kwa mwathirika wa tukio hilo.
Mtanzania huyo, Omega Mwaikambo (43)
alituma video na picha za mwili wa marehemu uliokuwa kwenye begi na
baadaye picha nyingine tano zikionyesha uso wa marehemu huyo.
Gazeti la mtandaoni la The Telegraph
limeandika kuwa Mwaikambo amekiri makosa ya kutuma mara mbili picha
zisizopendeza kwa umma katika mitandao ya kijamii mbele ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi ya Westminster jana.
Mwaikambo ambaye anaishi hatua chache
kutoka lilipo jengo la Grenfell akifanya shughuli za upishi, alishuhudia
jinsi jengo hilo lilivyoungua moto usiku na alikuwa ni miongoni mwa
wapishi waliowapikia chai wafanyakazi wa zimamoto walipokuwa wakizima
moto huo.
“Lakini juzi Jumatano asubuhi
alipoangalia miili hiyo nje ya nyumba yake alichukua picha kwa kutumia
simu yake aina ya iPad na kuzipakia kwenye mtandao wake wa Facebook,”
liliandika gazeti hilo.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Tom Little
amesema; “Anaishi karibu zaidi na mnara wa Grenfell, kama ambavyo
mahakama inajua janga hilo lilitokea Juni 14.”
Akitoa hukumu, Jaji wa mahakama hiyo,
Tanweer Ikram amesema; “Dunia nzima imeshtushwa na yaliyotokea hapa
kutokana na janga la moto, ni hali ya kutisha isiyostahimilika, wafu ni
lazima waheshimiwe.”
Ameongeza; “Ulichokifanya kupakia hizo
picha kwenye Facebook ni dhahiri kuwa hujaonyesha heshima kwa waathirika
wa tukio hilo, kuonyesha uso wake hadharani ni kosa kubwa na
halielezeki.”
Mpaka sasa watu zaidi ya 17 wanadaiwa
kufariki dunia kutokana na moto uliounguza jengo hilo refu na maarufu
Magharibi mwa Uingereza.