MAHAKAMA YAMALIZA MGOGORO WA TIMU YA STAND UNITED FC
HATIMAYE Mahakama ya wilaya ya Shinyanga imetoa hukumu yake kuhusiana na
kesi iliyokuwa imefunguliwa na kundi moja la wanachama lililojiita
Stand United Kampuni likiomba kumilikishwa timu hiyo kutoka mikononi mwa
kundi lingine la wanachama wa Stand United.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu mkazi Evodia Kyaruzi, alisema
baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili mahakama hiyo imetupilia
mbali pingamizi lililofunguliwa na upande wa walalamikaji (Stand
kampuni) na kuamua timu hiyo iendelee kumilikiwa na wanachama wenyewe.
Kyaruzi alisema kutokana na hali hiyo timu hiyo itaendelea kuwa chini ya
wanachama wenyewe kwa kutumia jina lake lilelile la Stand United
Football Club na kubariki rasmi uongozi uliokuwa umechaguliwa na
wanachama wenyewe chini ya menyekiti wao, Dkt. Ellyson Maeja na kwamba
wanachama ndiyo watakaokuwa na sauti ya mwisho kuhusiana na uendeshwaji
wake.
Akizungumza baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwenyekiti wa timu ya
Stand United FC, Dkt. Ellyson Maeja alielezea kufurahishwa na jinsi
mahakama ilivyotenda haki ambapo alisema kazi kubwa iliyopo mbele yake
hivi sasa ni kurejesha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama.
Alisema hakuna sababu ya wanachama wa Stand FC kuendeleza mgogoro
uliokuwepo na badala yake waungane kuwa kitu kimoja ili kuijenga timu
yao kwa kujitolea kwa hali na mali ikiwemo kutafuta wafadhili
watakaosaidia ili iendelee kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom
hapa nchini.
“Nimefurahi kwa jinsi mahakama yetu ilivyotenda haki, tunamshukuru
mwenyezi mungu kuona suala hili leo (jana) limemalizika, ukweli sisi
viongozi tuliochaguliwa na wanachama tulikuwa na wakati mgumu muda mfupi
baada ya kuchaguliwa kwetu, tulipambana na changamoto nyingi ikiwemo
kuwekewa pingamizi hili mahakamani,”
“Kwa hali hii nawaomba wanachama na wapenzi wote wa Stand United F.C
tuungane na kuwa kitu kimoja ili kuiendeleza timu yetu, ambayo kwa sasa
ni ya sita katika msimamo wa ligi, tutafute wafadhili wa kutusaidia ili
tuijenge kwa ajili ya msimu ujao iwe imara iweze kutwaa taji la ubingwa
badala ya timu kubwa za Simba na Yanga zilizozoeleka,” alieleza Maeja.
Maeja aliendelea kueleza kuwa hivi sasa wanakaribisha wafadhili wenye
mapenzi watakaotaka kuisaidia timu hiyo na kwamba wanachama wako tayari
kukubali timu iitwe jina lolote ikiwa chini yao ili mradi iendelee
kufanya vizuri katika medani ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.
source MALUNDE BLOG