Mahakama Yabariki Kina Shikuba Kupelekwa Marekani
Mahakama
imekubali maombi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison
Mwakyembe ya kutaka Watanzania watatu washikiliwe wakati wakisubiri
kibali cha kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha
na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.
Uamuzi
wa kuyakubali maombi hayo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha, baada ya kujiridhisha na
ushahidi na vielelezo vilivyotolewa mahakamani.
Kabla ya Hakimu Mkeha kutoa uamuzi huo, Shikuba alisema ni bora wakapelekwa Marekani kwa sababu wanaweza kupata haki yao.
“Ni bora tukapelekwa Marekani tunaweza kupata haki yetu, watu watatu tunatuhumiwa kwa kilo 1.78 za heroine, kweli hiyo?
“Tunaishi
kama wahujumu uchumi, hatujabadilisha nguo siku ya tatu, kesi Lindi
nimefutiwa na kilo 200 za heroine nakuja kushtakiwa Marekani kwa kilo
moja.
“Sina hata viatu, nimetolewa Lindi hivyo hivyo… nitakuwa mtu wa kwanza kuingia Marekani nikiwa nimevaa ndala,”alidai Shikuba wakati akisubiri Hakimu aingie mahakamani.
Kifungu
cha 8(3) cha Sheria ya Kusafirisha wahalifu kinasema hakimu
akishajiridhisha na ushahidi uliofikishwa mahakamani anampa taarifa
Waziri wa Katiba na Sheria kwa ajili ya kutoa kibali cha kuwasafirisha.
Hakimu
Mkeha akisoma uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, alisema
mahakama kabla ya kuamua ilijiuliza maswali kadhaa ikiwamo kama mashtaka
wanayohusishwa nayo wajibu maombi yako katika utaratibu wa kubadilisha
wahalifu.
Pia
mahakama ilijiuliza kama kuna mkataba kati ya nchi husika ambako baada
ya kuangalia imebaini kwamba kuna makubaliano ya kubadilishana wahalifu
kati ya nchi hizo mbili.
“Mahakama
imekubaliana na maombi yaliyowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria,
mahakama inatoa amri ya kuwashikilia wajibu maombi mpaka waziri
atakapotoa kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani,”alisema.
Hakimu
Mkeha alisema kama wajibu maombi watakuwa wanapingana na uamuzi huo,
mahakama inawapa nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 15.
Mwakyembe
aliwasilisha maombi Februari 15 mwaka huu, akiomba mahakama hiyo
kuamuru Kiongozi wa Taasisi ya Kusambaza Dawa za Kulevya nchini, Ally
Haji, maarufu Shikuba, Iddy Mfuru na Tiko Adam washikiliwe wakati
wakisubiri kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani kujibu tuhuma za
kula njama kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.
Jamhuri
iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki na katika
kuiridhisha mahakama iliwasilisha maombi pamoja na ushahidi dhidi ya
wajibu maombi, wa kuonyesha kujihusisha kwao katika matukio hayo.
Ushahidi
ulionyesha kwamba Marekani iliwachunguza wajibu maombi kwa miaka minne
na walitumia Dola za Marekani 10,000 kununua dawa hizo kutoka kwa
taasisi yao ili kubaini ukweli..
Wajibu
maombi ilibainika walikuwa wakisafirisha heroine kwa kutumia magari,
wakifikisha dawa hizo Marekani na kuwatumia watu kusambaza kwa kutumia
ndege binafsi na Shikuba ndiye kiongozi wa taasisi hiyo.
Kakolaki
alidai maombi yaliambatana na kiapo kilichoapwa na Richard Magnes
ambaye katika kiapo chake anadai wajibu maombi wanatuhumiwa kuingiza
dawa za kulevya zaidi ya kilo 1.78 Marekani.
Alidai
ushahidi katika kiapo hicho unadai aliwahi kukamatwa mbeba dawa(punda)
mwaka 2012, alizitoa kwa njia ya haja kubwa na alipohojiwa alimtaja
Shikuba kuwa alimpa dawa hizo.
Kakolaki
alidai tangu mwaka 2005 wajibu maombi wanatajwa na watuhumiwa
mbalimbali Marekani kwamba ndiyo wanaosambaza dawa hizo kwa kutumia
taasisi yao inayoongozwa na Shikuba.
Ushahidi
huo wa kiapo unadai Shikuba aliwafundisha miongoni mwa watuhumiwa
waliokamatwa, jinsi ya kubeba dawa hizo na kusafirisha na kwamba dawa
hizo zilikuwa zikiingia Tanzania kwa meli kupitia mwambao kwa
maelekezo ya Shikuba.