Taarifa Ya JWTZ Kuhusu Mauaji Ya Kondakta Mkoani Tanga
Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limesikitishwa na taarifa iliyotolewa
na gazeti la Tanzania Daima toleo Nambari 4438 la tarehe 28 Januari
2017, Habari leo la tarehe 29 Januari 2017 na baadhi ya vyombo vya
habari vikihusisha mauaji ya kondakta wa daladala na Wanajeshi Mkoani
Tanga.
Tunapenda
kuwataarifu wananchi kwamba kwa mujibu wa jeshi la polisi watuhumiwa
wanaoshikiliwa na Jeshi hilo ni wanne (4),mmoja kati yao ni Mwanajeshi
ambaye ni mzazi wa msichana anayetuhumiwa kusababisha tukio hilo.
Hivyo
Mwanajeshi huyo anashikiliwa kwa ajili ya kulisaidia Jeshi la Polisi
katika uchunguzi kwa kuwa tukio hilo lilifanyika nyumbani kwake.
Hakuna
Wanajeshi waliohusika katika tukio hilo kama ilivyoripotiwa na baadhi
ya vyombo vya habari, kambi za Jeshi wanaishi Wanajeshi pamoja na
familia zao hivyo kuhusisha moja kwa moja mauaji hayo na Wanajeshi
mkoani Tanga ni kuupotosha umma.
Wito
unatolewa kwa vyombo vya habari kuripoti habari zenye ukweli.Habari
zisizo za kweli zinapotosha umma na kujenga taswira potofu kwa wananchi
dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203,
Dar es Salaam,
Tanzania.