Waziri Mhagama aibana Halmashauri ya Meatu, aitaka kuwasaidia vijana
Halmashauri
ya Wilaya ya Meatu imeombwa kuwatengenezea mfumo wa kibiashara vijana
wa Meatu Milk ili waweze kuboresha na kuendeleza bidhaa ya maziwa
yanayotengenezwa na kiwanda hicho.
Rai
hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira, na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea
kiwanda Meatu Milk na kufungua jiwe la uzinduzi wa mradi wa kusindika
maziwa katika Halmashauri ya Meatu Mkoani Simiyu.
Mhe.
Jenista amesema kuwa mradi wa usindikaji maziwa ni mradi utakaowavuta
wafugaji wengi kuondokana na tatizo la kuangaika na mifugo yao kwa
sababu soko la maziwa litakua la uhakika hivyo kupanua uchumi wa Wilaya
ya Meatu.
“Twendeni
tukafungue matendo kwa vijana wa Tanzania tuwaondoe katika mitazamio ya
fikra hafifu na kuwapeleka katika kujitegemea ili wajenge taifa letu na
kuondokana na dhana ya umasikini waliyoikumbatia kwa muda mrefu,”
alisema Mhe. Jenista.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amemwambia Mhe. Jenista kuwa
hatamualika Simiyu kufungua makongamano na warsha za ujasiriamali bali
ataendelea kumualika katika Mkoa wake kwa ajili ya kufungua viwanda
vingine vya vijana kwani mkoa umejipanga kuwa na viwanda vya kutosha
vitakavyozalisha malighafi zote zinazopatikana Mkoani Simiyu.
Mhe.
Mtaka amewaomba wana Meatu na wananchi wote wa Simiyu kuwa na uthubutu
wa kubuni miradi endelevu ili waweze kujivunia vya kwao kwani Mkoa
umejichagua kuwa pacha wa kutekeleza Ilani ya uchaguzi sambamba na Rais
Mhe. John Pombe Magufuli na kuweza kuiongoza nchi kufukia malengo ya
Ilani ya Chama tawala kwa vitendo.
Aidha
Mwenyekiti wa Meatu Milk Bibi. Lightness Benedictor amesema kuwa mradi
umegharimu kiasi cha shilingi 34,903,000 ambapo shilingi 10,000,000 ni
michango ya wanachama kutoka kwenye gawio ya fedha za mkopo uliotolewa
na Wizara kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kiasi cha shilingi
24,902,000 ni mkopo kutoka kwenye asilimia tano ya mapato ya ndani ya
Halmashauri ya fedha zilizotengwa kuwezesha vijana.
Mradi
wa Meatu Milk unatekelezwa chini ya mpango mkubwa wa kiuchumi wa Mkoa
wa Simiyu wa kuanzisha bidhaa moja kwa Wilaya moja ili kutekeleza Ilani
ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 ya kuwa na
Tanzania ya viwanda.