MTENDAJI MKUU TEMESA AWAFUKUZA KAZI WAFANYAKAZI SITA NA KUWAPA ONYO WAWILI WA KIVUKO CHA MV KOME MWANZA.
Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi
Mussa Mgwatu (kushoto) akisikiliza taarifa ya kituo cha TEMESA Mkoa wa
Mwanza kutoka kwa Meneja wa TEMESA mkoani humo Mhandisi Ferdinand
Mishamo.
Abiria wakiteremka katika Kivuko cha Mv Kome II kinachotoa huduma kati ya Nyakarilo na Kome wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Mtendaji Mkuu TEMESA Dkt. Mussa
Mgwatu amemuagiza Meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo
kuwafuta kazi mara moja watumishi sita wa kivuko cha Mv Kome kuanzia
11/10/2016 pamoja na kuwapa onyo kali watumishi wengine wawili wa kivuko
hicho kwa kuondoka katika eneo la kazi bila ruhusa ya mkuu wao wa kazi.
Ametoa agizo hilo wakati
alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha TEMESA mkoani Mwanza na
kutembelea kivuko cha Mv Kome kinachotoa huduma ya usafiri kati ya Kome
na Nyakarilo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Dkt Mussa Mgwatu pia amemwagiza
Meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo kuhakikisha
wafanyakazi wa karakana na kivuko wanawajibika ipasavyo ili kuondoka na
uzembe kama uliojitokeza.
“Hatuwezi kuvumilia uzembe namna
hii watumishi wanaamua tu kuondoka eneo la kazi bila kupata ruhusa
kutoka kwa wakuu wao hii sio sawa kabisa na nakuagiza Meneja hawa
watumishi waache kazi mara moja” alisisitiza Dkt Mgwatu.
Aidha Dkt Mussa Mgwatu amemwagiza
Meneja wa TEMESA Mwanza kuajiri watumishi wengine ili kujaza nafasi
zilizoachwa wazi kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji wawatumishi
watakao waajiri.
Kwa upande Meneja wa TEMESA Mwanza
Mhandisi Ferdinand Mishamo alikiri kuwa hakukuwa na ruhusa yoyote ya
maandishi iliyotolewa kwa watumishi kutokuwepo kazini siku hiyo.
“Mtendaji sina barua yoyote kutoka
kwa watumishi hawa iliyofika kwangu kuomba ruhusa ya kutokuwepo katika
kituo cha kazi.” alisisitiza Mhandisi Mishamo.
Mhandisi Ferdinand Mishamo amewaja
watumishi waliachishwa kazi kuwa ni walinzi wanne Bw. Apolinary
Kapulula, Bw. Marwa Nchagwa , Bw. Msomi Stanley na Joseph Mtokambali,
wengine ni Bw. Baharia Geofrey Biseko na Mkusanya Mapato wa kivuko hicho
Bw. Elisha Mbondo.
Amewataja Watumishi wanaopewa onyo
kali ni Mkuu wa Kivuko cha Mv Kome Bw.Elias Mabushi na dereva wa kivuko
hicho Bw.Juma Bugingo.
Dr. Musa Mgwatu yupo katika ziara
ya kutembelea vituo vya TEMESA vilivyopo Kanda ya Ziwa ili kubaini
changamoto zilizomo na kuzitafutia ufumbuzi.