Waingereza watoa msaada kwa wakimbizi 236,000
Ni
kutokana na mchango mkubwa wa Paundi za Uingereza milioni 1 (Dola za
Marekani milioni 1.3) kutoka katika Shirika la Misaada la Uingereza
(Department for International Development –DFID), kwamba Shirika la
Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeweza, walau kwa
muda, kusitisha mpango wa kupunguza kiasi cha mgao wa chakula uliopangwa
kwa ajili ya wakimbizi nchini Tanzania.
WFP
ilikuwa imepanga kupunguza kiasi cha mgao kuanzia Oktoba kwa karibu
robo milioni ya wakimbizi kutokana na kukosekana kwa fedha za kuendeshea
shughuli za WFP za kuhudumia wakimbizi nchini Tanzania. Sasa – walau
kwa muda huu – shughuli hizi zitaendelea kama kawaida.
“Uingereza
inaungana na Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa katika kusaidia
ukarimu mkubwa wa Serikali na watu wa Tanzania wa kuwakaribisha wale
wanaotafuta usalama kutokana na mapigano nchini Burundi na ukanda wa
Maziwa Makuu,” alisema Vel Gnanendran, ambaye ni Mkuu wa DFID. “Kwa
hiyo, tunatoa mchango wa nyongeza mara moja wenye thamani ya Paundi
milioni 1 ili kuisaidia WFP kuendelea kutoa chakula kwa idadi inayokuwa
ya wakimbizi wanaowasili nchini Tanzania. Nyongeza hii inafanya jumla ya
mchango wetu kwa WFP kufikia Paundi milioni 6.5 tangu mgogoro huu
uanze.”
WFP
husambaza chakula kinachookoa maisha kwa wakimbizi wapatao 236,000
wanaoishi katika kambi tatu mkoani Kigoma, kaskazini magharibi mwa
Tanzania. Wakimbizi wanategemea msaada huu, ambao ni pamoja na mahindi,
kunde, mafuta ya kupikia, chumvi na mchanganyiko wa uji wenye
virutubisho.
“WFP
inatoa shukrani za dhati kwa DFID kwa mchango wao katika kipindi hiki
muhimu,” alisema Michael Dunford, Mwakilishi wa Nchi wa WFP nchini
Tanzania. “Wakati ambapo fedha zaidi za nyongeza zinahitajika haraka ili
kukidhi mahitaji ya wakimbizi hadi kufikia mwisho wa mwaka huu,
tunathamini sana mchango huu mkubwa.”
Licha
ya kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji ya kikalori ya kila siku ya
wakimbizi, WFP hutoa chakula kilichopikwa katika vituo vya mpito na
kupokelea wakimbizi na vituo vya afya. Katika kambi za wakimbizi, WFP
pia husaidia akina mama wajawazito na wale wanaonyonyesha, na pia watoto
wenye utapiamlo wa kiwango cha kati walio na umri wa chini ya miaka
mitano kwa kuwapatia unga wenye virutubisho au mchanganyiko wa uji
ulioongezewa virutubisho.
Kila
siku, mamia ya wakimbizi kutoka Burundi huwasili katika mpaka wa
Tanzania, hasa kutokana na kuendelea kwa mapigano nchini mwao. WFP
inamudu kutimiza wajibu wake kutokana na misaada itokayo kwa wahisani.
Lakini kutokana na kuendelea kumiminika kwa wakimbizi, Shirika lina hali
ngumu ya kifedha. Michango isipoongezeka, usalama wa chakula na lishe
wa wakimbizi unaweza kuwa katika hatari kubwa.
Ili
kuendeleza shughuli za kuwahudumia wakimbizi hadi mwisho wa mwaka, WFP
inahitaji Dola za Marekani milioni 7.6. Jumla ya Dola za Marekani
milioni 63.6 zinahitajika hadi kufika Agosti, 2017.