UVCCM WAMTEMBELEA MAJERUHI WA SCORMPION
UMOJA wa Vjana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM), umelihimiza Jeshi la polisi nchini kutambua kuwa
ujambazi, wizi wa kutumia silaha na uporaji bado ni tatizo linalohitaji
kushughulikiwa kwa nguvu zote kama ambavyo nchi ilisimama na kutekeleza
operesheni mbalimbali za ukombozi.
Pia, umesisitiza kuwa usalama wa
raia na mali zao unahitaji kulindwa ili kuepusha vifo, hasara,
unyang’anyi wa mali na vilema vya maisha kutokana na matukio yanayoweza
kuwakumba wasio na hatia mijini na vijijini.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM,
Shaka Hamdu Shaka, alieleza hayo jana alipomtembelea kumjulia hali
majeruhi Said Ally, Mabibo Hostel.
Saidi alijeruhiwa maeneo
mbalimbali ya mwili wake ikiwa ni pamoja na kutobolewa macho katika
tukio wizi wa kutumia silaha Buguruni mjini Dar es Salaam, Septemba
mwaka huu.
Shaka alisema tatizo la uhalifu,
unyang’anyi, uporaji na ukwapuaji mali kwa kutumia nguvu na silaha,
linahiaji kutazamwa kwa kina na upana unaostahili na vyombo vyenye
dhamana vinavyosimamia usalama wa raia na mali zao.
Alisema kuna haja ya polisi
kubuni mbinu mpya za kukabiliana na makundi ya wezi, waporaji na
majambazi kabla hawajaleta madhara na hasara kama ilivyomtokea Said
ambaye sasa ni amesababishiwa ulemavu wa kudumu wa kutoona.
“Kila siku mbinu za uhalifu,
ujambazi, wizi wa kutumia nguvu na silaha hubadilika, jukumu la
kupambana na matukio hayo hatari ni la polisi kwa kushirikiana na raia
wema, janga hili likiachwa wananchi wataishi kwa mashaka na hawatajituma
kujiletea maendeleo,”alisema Shaka.
Alisema ikiwa wananchi wanajituma
kwa bidii kutafuta fedha na kubuni miradi ya kiuchumi halafu majambazi
na wanyang’anyi wanapora na kumfilisi aliyetafuta ndani ya saa chache,
hilo linaweza kuwatia hofu mwananchi na wajasiriamali na kuwafanya
washindwe kujituma kikamilifu jambo ambalo litakuwa na madhara makubwa
katika kuzalisha mali na kukuza uchumi.
Akizungumza kwa masikitiko na
huzuni kubwa , Shaka alisema tamaa ya kupata utajiri kwa njia haramu kwa
mtu mmoja mmoja au kikundi, kumemsibaishia hasara ya maisha dhidi ya
Said ambaye kwa sasa amekoseshwa uwezo wa kuendelea kupiginia maendeleo
yake ya kiuchumi na taifa kwa ujumla.
“Ifike mahali tatizo la uhalifu,
ujambazi na uporaji lishughulikwe kama harakati za mapambano dhidi ya
maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukoma na kifua kikuu, tukilipuuza
tatizo hili litaigharimu jamii na kuwaletea kadhia ya umasikini wananchi
na Tanzania kwa ujumla,”alieleza.
Kwa upande wake majeruhi Said
aliishukuru UVCCM kwa kuonyesha kumjali na kufika kumjulia hali kutokana
na janga lililomkuta na kumpa msaada huku akiwahimiza waendelee
kuikumbusha serikali isimuache kwa sababu amedhulumiwa utu wake na watu
aliowatuhumu kuwa ni majambazi bila ya hatia wala kosa lolote.
Said alisifu ujio huo wa ujumbe
kutoka Makao Makuu ya UVCCM Taifa lioongozwa na Shaka, Mwenyekiti wa
UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam Omar Matulanga na makatibu wa umoja huo
kutoka wilaya tano za mkoa huo.
Alisema akiwa kijana amefarijika
kutembelewa na vijana wenzake huku akiwahimiza wasimchoke kwa sababu
sasa amekuwa kipofu na hajimudu tena kimaisha.