Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya ndoa za utotoni kwa wasichana waliochini ya umri wa miaka 18.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jinsia, Wazee na Watoto, Magreth Mussai wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike duniani yanayofanyika Oktoba 11 kila mwaka, amesema takwimu zinaonyesha kuwa mkoa huo unaongoza kwa asilimia 59.
Mussai amesema kufuatia mkoa huo kukithiri ndoa za utotoni, ndiyo sababu ya wizara ya afya kuuchagua kufanya maadhimisho hayo kitaifa.
Hata hivyo, amesema mkoa unaofuata kwa kukithiri ndoa za utotoni ni Tabora kwa asilimia 58, Mara 55, Dodoma 51 wakati Dar es Dalaam ikiwa na asilimia 19.
Amesema sababu inayopelekea familia nyingi kuwaoza mabinti zao chini ya umri wa miaka 18 ni hali ngumu ya maisha na kwamba wazazi huitumia njia hiyo kujipatia fedha kwa kupata mahali.
Mussai amesema serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua kuwa ndoa za utotoni zina athiri kiafya na kimwili watoto hao.
Ambapo ameitaka jamii kuwajibika ili kuhakikisha kwamba watoto wa kike hawaozeshwi chini ya umri wa miaka 18.