Mkali wa Ngoma za Jadi Tukuyu kupatikana Octoba, 8, kupata nafasi ya kusoma Chuo cha Sanaa Bagamoyo
Tamasha
kubwa la ngoma za jadi la Tulia litakalojumuisha zaidi ya vikundi vya
ngoma 84 kutoka wilaya za Rungwe, Busokelo na Kyela linatarajiwa
kufanyika tarehe 7 hadi 8 ya mwezi huu wa kumi katika viwanja vya
Tandale wilayani Tukuyu.
Tamasha
hilo ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza, litajumuisha zaidi ya ngoma
za aina tisa huku baadhi ya ngoma zitakazoshiriki ni pamoja na
Ipenenga, Ingo’ma na Maghosi.
Akizungumzia
tamasha hilo, Naibu Spika wa Bunge na mwanzilishi wa tamasha hilo, Dkt.
Tulia Ackson amesema lengo la tamasha hilo ni kukuza na kuendeleza
tamaduni hasa za ngoma za asili.
“Ngoma
za asili zina sehemu kubwa katika utamaduni wetu, na ndio maana ni
muhimu sana kama taifa tutakajikita katika kuhakikisha zinatambulika na
pia zinaendelezwa,” alisema Dkt.Tulia.
Akielezea
zaidi kuhusu ngoma hizo Dkt Tulia alisema lengo la tamasha la ngoma za
jadi ni kuzifanya ngoma hizo zijulikane, na pia kuzipa umuhimu katika
jamii na hivyo kuzifanya zisipotee.
“Tamasha
pia litatoa fursa ya kiuchumi kwa vijana watakaoshiriki tamasha hilo
kwa wao kuanza kuzitazama ngoma kama chanzo cha kujipatia kipato,”
alisema Dkt. Tulia.
Mashindano
hayo yaliyoanza katika ngazi ya kijiji, kata, halmashauri na kanda,
huku jumla ya vijiji 393 vikichuana kupata fursa ya kushiriki katika
kilele cha matamasha hayo, yatahudhuriwa wageni mbalimbali kama mabalozi
kutoka nchi mbalimbali pamoja na wakurugenzi na wawakilishi kutoka
makampuni mbalimbali.
Mshindi
wa kwanza wa mashindano hayo atarekodiwa albamu ya nyimbo zake kwenye
DVD, pamoja na ufadhili wa kusomeshwa katika chuo cha Sanaa cha
Bagamoyo.
Mshindi wa pili atapata mashine ya kusaga na watatu atapata zawadi ya bodaboda.