SERIKALI YATOA TAMKO KWA WATUMISHI WA UMMA KUJITOKEZA KUSAJILIWA VITAMBULISHO VYA TAIFA KABLA YA OKTOBA 31, 2016
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya
habari mkoani Dodoma kuhusu mwenendo wa zoezi linaloendelea la usajili
wa Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma. Katikati ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mh. Angellah J. Kairuki (Mb) na Bi. Rose Mdami, Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano na Hifadhi Hati, akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu
NIDA
Katikati ni Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) Akisisitiza jambo wakati
akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu zoezi la kusajili
watumishi wa Uma nchi nzima. kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah J. Kairuki
(Mb) na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja
Jenerali Projest Rwegasira
Baadhi ya waandishi wa Habari
nchini wakisikiliza kwa makini ufafanuzi unaotolewa na Mawaziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora; kuhusu usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa
Umma zoezi linaloendelea nchi nzima
Baadhi ya waandishi wa Habari
walioshiriki mkutano wa tathmini ya mwenendo wa Usajili Vitambulisho vya
Taifa kwa watumishi wa Umma; mkutano uliofanyika ukumbi wa Kambarage,
jengo la Hazina Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) akiweka saini kitabu cha wageni
alipotembelea ofisi za Usajili za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
mkoani Dodoma, kukagua shughuli za usajili Watumishi wa Umma kabla ya
kuzungumza na waaandishi wa habari kutoa tathmini ya mwenendo wa zoezi
hilo
Waziri akipokea maelezo ya namna
shughuli za usajili zinavyo ratibiwa na ofisi ya usajili Wilaya ya
Dodoma Mjini ; alipofanya ziara ya ukaguzi na kukutana na viongozi na
watumishi wa Umma waliofika kupata huduma
……………………………………………
Serikali imewataka watumishi wote
nchini walioajiriwa na Serikali, yakiwemo mashirika ya Dini na Taasisi
nyingine ambazo haziko kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali
lakini zinapata ruzuku kutoka Serikalini; kuwa wamesajiliwa katika
zoezi la Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma linaloendelea
kote nchini, kufikia Oktoba 31, 2016.
Agizo hilo limetolewa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mh. Angellah J. Kairuki (Mb) alipozungumza na waandishi wa habari mjini
Dodoma, katika mkutano wa pamoja ulioitishwa kati ya Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi na Waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora.
Bi Kairuki amesisitiza; “waajiri
na watumishi watakaoshindwa kutekeleza zoezi hili watachukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo”
Akifungua mkutano huo uliolenga
kutoa tathmini ya mwenendo wa zoezi linaloendelea la Usajili wa
Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma lilioanza nchi nzima tangu
Oktoba 03, 2016, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu L. Nchemba
(Mb) amesema mpaka sasa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
imefanikiwa kusajili zaidi ya asilimia 50% ya watumishi wote nchi nzima
na baadhi ya mikoa kukamilisha usajili kwa zaidi ya asilimia 95%.
Ameutaja mkoa wa Geita kuwa mkoa unaoongoza kwa kufanya vizuri katika
zoezi hilo
Amesema pamoja na kuwepo kwa
changamoto mbalimbali zilizokwamisha zoezi hilo kukamilika kwa wakati
uliopangwa; Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, wameamua kuongeza muda wa kukamilisha zoezi hilo kwa
wiki mbili zaidi hadi Oktoba 31, 2016.
Amewataka watumishi kuondokana na
upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watumishi kwamba zoezi hilo
limelenga kuhakiki vyeti na badala yake wajitokeze kwa wingi kusajiliwa
kwani Serikali imelenga kuunganisha taarifa za mfumo wa mishahawa wa
Serikali na NIDA, ili mbali na kutatua tatizo la watumishi hewa; kupitia
mfumo huu wa kielektroniki unaomtambua mtu kwa alama zake za
kibaiolojia kuwa na maslahi mapana kwa taifa na kwa watumishi; kwa
kuunganisha mifumo mingine ya Serikali ukiwemo mfumo wa Kodi, mifuko ya
Hifadhi za Jamii, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Bima ya Afya,
Uhamiaji, RITA Na Benki ili kutoa manufaa mapana kwa mtumishi.
Amelipongeza Jeshi la Wananchi wa
Tanzania kwa kuwezesha kusambazwa kwa vifaa vya usajili nchi nzima,
Ofisi ya Rais TAMISEMI, Taasisi na Mashirika yote ya Serikali waliojitoa
kufanikisha zoezi la Usajili.
Kupitia zoezi la Usajili
Watumishi wa Umma, Tayari NIDA imefungua ofisi za usajili nchi nzima,
ngazi ya Wilaya kusogeza karibu zaidi huduma inayotolewa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Waziri Mwigulu Pindi zoezi la usajili watumishi
litakapokamilika usajili wa wananchi utaanza mara moja nchi nzima kwani
zoezi la usajili vitambulisho vya Taifa limelenga kila mwananchi, Mgeni
anayeishi kihalali nchini na Mkimbizi.