Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib
akizungumza na wanachama wa mtandao huo wakati wa mkutano wa kuchangia
maafa ya tetemeko la ardhi, Kagera.Picha na Mpiga picha wetu.
Mwanachama wa SHIWATA, Hamisi
Kiondo akichangia hoja ya namna ya kusaidia waliopatwa na maafa Kagera.
(Picha na Mpiga Picha Wetu).
…………………………………………………………….
Mtandao wa Wasanii Tanzania
(SHIWATA) unatarajia kukabidhi mchango wa maafa ya tetemeko la ardhi kwa
wananchi wa mkoa wa Kagera baada ya siku ya awali iliyokuwa imepangwa
ya Oktoba 14, 2016 ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kfo cha Mwalimu
Nyerere kuingiliana na ratiba nyingine za kitaifa.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim
Taalib akizungumza katika mkutano wa wanachama jana alisema mpaka sasa
fedha ambazo zinatarajiwa kukabidhiwa ni sh. 600,000 ambazo kati ya hizo
100,000 zimechangwa na wanachama katika mkutano huo.
Alisema wakati maandalizi ya
kukabidhi fedha hizo ukiendelea siku hiyo ambayo SHIWATA imetenga kwa
ajili ya kufanya kazi za kumuenzi baba wa Taifa, Nyerere viongozi wa
kitaifa ambao walikuwa wapokee mchango huo watakuwa mkoa wa Simiyu
katika sherehe ya kuzima Mwenge wa Uhuru.
Katika mkutano huo wanachama
waliahidi kuendelea kuchangia matukio yote ya kijamii na wengi wameahidi
kuwasilisha vifaa mbalimbali na nguo kwa waathirika wa tetemeko la
ardhi Kagera.
Wakati huo huo SHIWATA imetoa ofa
ya Sh. Mil. 3.2 kwa wanachama wake watakaojenga nyumba za kuishi katika
kijiji chao cha Mwanzega Mkuranga.
Akifafanua kuhusu ofa hiyo,
Taalib alisema gharama za kusafirisha vifaa vya ujenzi, gharama za
kusafisha eneo la kujenga na ekari moja ya kulima bustani watapewa bure.
Alisema kasi ya wanachama kujenga
na kuhamia kijijini inaridhisha mpaka sasa nyumba 200 zimekamilika na
nyingine zinaendelea kujengwa.
Taalib huduma za jamii kijijini hapo zinafanyiwa kazi ambapo huduma ya maji safi na salama ya kisima kirefu itapatikana mapema.