KAMPUNI YA KITANZANIA KUUNDA GARI LA KWANZA DESEMBA 2016
Waziri mkuu
Kassim Majaliwa akipokea picha yenye sura yake kutoka kwa mwenyekiti
wa kampuni ya Ujenzi ya CRCC ya China Bw. Fengchao kulia ni katibu wa
chama cha ushirikano na maendeleo kati ya china na Tanzania Bwana Joseph
Kahama ujumbe huo kutoka china ulifika ofisini kwa waziri mkuu
Magogoni jijini Dar es salaam kwa mazungumzo ya kikazi na kutoa pole kwa
tetemeko la Kagera
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wageni hao.
………………………………………………………………………….
*Wapanga kulizindua kabla ya Krismas mwaka huu
KAMPUNI ya Simba Motors imesema ina mpango wa kujenga kiwanda cha kuunganisha magari aina ya pick-up ambacho kitaanza kuzalisha magari kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
Ahadi hiyo imetolewa leo mchana
(Jumatatu, Oktoba 10, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw.
Jitesh Ladwa mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mazungumzo
yaliyofanyika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Tumeamua kuunda magari aina ya pick-up
kwa sababu ya mahitaji makubwa yaliyopo nchini. Takwimu zinaonyesha
kuwa, kwa mwaka Tanzania inanunua magari ya aina hii zaidi ya 4,000.
Katika nchi za SADC mahitaji ni pick-up 35,000 kwa mwaka. Tutaanza na
mtaji wa dola za Marekani milioni 200 na tumeomba ekari 200 katika eneo
la EPZ,” amesema.
“Eneo la kiwanda cha kuunganisha
magari peke yake linahitaji ekari 50, kwa hiyo tukiweka na yadi za
kupaki magari, eneo la viwanda vingine, eneo la kushusha na kupakia
makontena yatakayokuwa yakisafirishwa kwenda nchi jirani, ni lazima
tutahitaji eneo kubwa zaidi,” amesisitiza.
Amesema mradi huo wa majaribio,
utaanza kwa kutengeneza magari 20 kila mwezi na kwamba kazi ya
utengenezaji magari itaongezeka na kufikia 1,000 na baadaye 5,000 kwa
mwaka. “Tunataraji gari la kwanza litazinduliwa kabla ya Krismasi, mwaka
huu,” amesema.
Bw. Ladwa amesema uundaji wa
magari hayo aina ya Foton-Tunland utafanyika kwa ubia baina ya kampuni
yao, SUMA-JKT na kampuni Foton International ya China kwa kutumia
teknolojia ya Kichina na kwamba magari hayo yanayotumia 4-Wheel Drive, yana uwezo wa kupita kwenye barabara za aina zote.
Akizungumza katika kikao hicho,
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Bw. Aatish Ladwa, amesema
mradi utakapoanza, mbali ya kutoa ajira kwa Watanzania, utawezesha pia
kujengwa kwa viwanda vingine vitakavyotengeneza matairi ya magari, vioo,
taa, bumpers, viti na filters.
“Tunataraji kujenga uwezo wa
wahandisi wazawa, uhamishaji wa ujuzi kwa mafundi wa Kitanzania
(technology transfer), kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho, kupunguza
gharama za uzalishaji, kutekeleza amza ya Serikali ya kuifanya Tanzania
kuwa ni nchi ya viwanda, kuongeza ajira kwa wanajeshi, na kuwezesha
upatikanaji wa vipuri vya magari kwa urahisi na kupunguza uagizaji wa
bidhaa kutoka nje ya nchi.”
“Kiwanda kitaajiri wafanyakazi
1,500 kwa kuanzia ambao watakuwemo mafundi na watoa huduma mbalimbali,
lakini katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano, tunataraji kuongeza
wafanyakazi wengine 5,000 wakati uzalishaji ukiwa umepamba moto,”
amesema.
Kwa upande wake, akizungumza mara
baada ya kulikagua gari la mfano aina ya Foton-Tunland, Waziri Mkuu
amesema anawakaribisha kwenye uwekezaji huo hasa ikizingatiwa kuwa
magari hayo yana uwezo wa kupita kwenye maeneo ya vijijini ambako
barabara zake siyo nzuri.
“Ofisi za Serikali zinayahitaji
zaidi haya magari, hospitali zetu za wilayani nazo pia zinayahitaji haya
magari ili yaweze kutoa huduma za chanjo kwa watoto, huduma za UKIMWI,
kampeni za kupambana na malaria, na huduma kwa mama wajawazito huko
vijijini,” amesema.