DC Kilombero awaagiza Wakurugenzi kuwachukulia hatua watendaji watakaoruhusu ndoa za utotoni

index
 
 
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro, James Ihunyo amewaagiza Wakurugenzi kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wa Vijiji, Kata na Mitaa watakaothibitika kuwa na ndoa za utotoni katika maeneo yao ikiwa ni njia mojawapo ya kutokomeza tatizo hilo.
 
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Wilaya hiyo alipokuwa akisoma hotuba wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyoandaliwa na Shirika la Plan International na kufanyika katika Kijiji cha Ihenga, Mkoani humo.
 
Ihunyo amesema kuwa pamoja na Mkakati wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 kuwa na lengo la usawa wa kijinsia na kuhakikisha haimuachi msichana nyuma katika suala zima la maendeleo lakini kama hakutokuwa na ufuatiliaji na utoaji wa taarifa juu ya changamoto za wasichana mikakati hiyo haitafanikiwa.
 
“Ili kuhakikisha tunakomesha ndoa za utotoni na kuhakikisha tunafikia malengo ya Sera ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030, nawaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote wa wilaya hii ambao watathibitika kuwa na wasichana walioolewa chini ya umri wa miaka 18 katika maeneo hayo”, alisema Ihunyo.
 
Pia, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha kuwa wale wote wanaowaoa au kuwaoza wasichana chini ya umri wa miaka 18 wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
 
Aidha, amewaasa wasichana kujiepusha na mazingira hatarishi yanayowapelekea kupata mimba au kuolewa kabla ya umri wao na kuwasisitiza kutoa taarifa hata kwa siri kwenye ofisi za Serikali ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
 
“Ndugu wananchi, tatizo la kunyanyasa na kuwabagua wasichana bado ni kubwa duniani, kutokana na utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) linasema kuwa katika kila dakika 10 mahali fulani hapa duniani msichana anafariki kutokana na ukandamizaji hivyo,ushirikiano wa hali ya juu unatakiwa kutoka kwa Serikali, Mashirika, wazazi pamoja na watoto wa kike wenyewe”, aliongeza Ihunyo.
Powered by Blogger.