Chama cha ACT Wazalendo kimefanya mkutano wake mkuu wa kidemokrasia jijini Dar es salaam
Chama cha ACT Wazalendo kimefanya mkutano wake mkuu wa kidemokrasia jijini Dar es salaam ikiwa ni utekelezaji wa katiba ya chama chao ambayo inawataka kila mwaka kufanya mkutano kama huo ambao wanachama wote hai wanaruhusiwa kuhudhuria
.
Mkutano huo ambao umehudhuriwa na wanachama kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao wamejigharamia ulikuwa na ajenda kuu tatu ikiwamo ya kujadili kuhusu hali ya kisiasa nchini, mjadala kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020, pamoja na mjadala kuhusu suala zima la katiba mpya ambalo kwa hivi sasa linaonekana kama limekufa.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuwasilisha mada yake kwenye mkutano huo, Kiongozi wa ACT Zitto Kabwe amesema chama chao kiliamua kuingiza utaratibu wa mkutano huo kufanyika kila mwaka kwenye katiba yao baada ya kutambua kuwa bila kufanya hivyo kunakuwa na pengo kubwa kati ya chama na wanachama na hivyo kutoa mwanya kwa viongozi kuweza kugeuza chama kama mali yao binafsi.
Mkutano huo ambao ni wa kisera utakuwa unafanyika kila mwaka kwenye miji tofauti tofauti kulingana na wanachama wenyewe watakavyopigia kura wakati wa mkutano.