UGUMU WA MAISHA WANAUME WADAIWA KUZIKIMBIA FAMILIA ZAO
Wananchi wa eneo la Msitu wa Tembo, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuwajengea bwawa la kunyweshea mifugo pamoja na kuwasaidia kupata maji kwa ajili ya shughuli nyingine za kiuchumi, wakieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukame inayowaathiri katika maisha yao ya kila siku.
Wamesema hali ya ukame imeathiri shughuli zao za uvuvi na ufugaji, ikiwemo kupunguza uwezo wa bwawa kutunza samaki ambao ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya kipato kwa wananchi hao. Kwa sababu hiyo, wameomba Halmashauri kuwawezesha kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ili waanzishe biashara na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.
Wananchi hao wameeleza kuwa ugumu wa maisha unaochangiwa na ukame umefanya baadhi ya wazazi kushindwa kumudu majukumu ya familia, hali inayodaiwa kuchangia baadhi yao kukimbia na kutelekeza familia zao. Wamesema hali hiyo inawaathiri watoto kwa kukosa malezi ya kutosha kutoka kwa wazazi wote wawili.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyumba ya Mungu, Afisa Maendeleo ya Jamii, Lydia Mbalila, na Afisa Ustawi wa Jamii wilayani Simanjiro, Lydia Ibrahim Juma, wamesema msingi wa malezi bora unaanzia kwa wazazi. Aidha, wamesisitiza umuhimu wa wazazi kuhakikisha watoto wanasomeshwa bila ubaguzi, hususan kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.