MZAZI AMTANDIKA VIBOKO MWALIMU MKUU
Mwananchi wa Kijiji cha Lembapuli, Kata ya Loolera wilayani Kiteto, Saitabahu Mirakwa anadaiwa kumshambulia kwa fimbo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lembapuli baada ya kutoridhishwa na hatua ya mwalimu huyo kumuadhibu mtoto wake wa kiume anayesoma Darasa la Tatu.
Akizungumza na
wananchi wa Lembapuli katika mkutano wa hadhara Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,
Remidius Mwema, ameagiza Serikali ya
Kijiji kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha mtuhumiwa anapatikana.
Mwema amesema ataulchukua hatua dhidi ya Kamati ya Usalama ya Serikali ya Kijiji endapo itabainika kuwa baadhi ya viongozi walihusika katika kumficha au kumtorosha mtuhumiwa huyo huku akieleza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba vitendo vya kuwashambulia walimu vinaweza kuwavunja moyo katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wao, Wazee
wa Kimila (Malaigwenani) kutoka Kijiji cha Lembapuli wameahidi kushirikiana na
Jeshi la Polisi kuhakikisha mtuhumiwa huyo anapatikana na kuchukuliwa hatua za
kisheria. Wamesema wananchi wanapaswa kufuata taratibu na sheria badala ya kujichukulia
sheria mkononi.
Diwani wa Kata
ya Loolera, Sokoine Edward Oltus, amelaani tukio hilo na kuahidi kushirikiana
na wananchi pamoja na vyombo vya dola kuhakikisha mtuhumiwa anapatikana ili
sheria ichukue mkondo wake.
Aidha Katika hatua nyingine
baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wamemshukuru Mkuu wa Wilaya ya
Kiteto kwa kuchukua hatua ya kukemea tukio hilo na kusisitiza umuhimu wa
kuheshimu sheria, huku wakitoa wito kwa viongozi kuchukua hatua za haraka dhidi
ya vitendo vinavyokiuka sheria na kuhatarisha usalama wa jamii.