RC MARA ATOA MASAA 24 FAMILIA YA RUHUMBIKA KULIPWA FIDIA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evance Mtambi, ametoa masaa 24 kukamilishiwa malipo ya fidia ya ardhi na makazi ya familia yam zee Ruhumbika Machumu ambae nimkazi wa kijiji cha Chirorwe ili kuhitimisha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya familia hiyo na Kampuni ya Wakazi Mining Limited inayojishughulisha na uchimbaji wa madini katika eneo hilo.
Kanali Mtambi ametoa maelekezo hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Chirorwe, ambapo amesisitiza kuwa baada ya majadiliano na makubaliano ya pande zote kukamilika, familia hiyo inapaswa kulipwa fidia ya shilingi milioni 40 kama ilivyokubaliwa ili waweze kuondoka katika eneo hilo na kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Hivi karibuni Familia
ya Mzee Ruhumbika ilitoa malalamiko mbele ya waziri mkuu wa jamhuri ya muungano
wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba kuomba kulipwa fidia ambapo alimwagiza afisa
madini mkoa wa Mara kukaa na familia hiyo nakisha kutoa mrejesho kwenye ofsi ya
mkuu wa mkoa wa Mara na sasa amefika katika eneo hilo nakisha kusikiliza pande
zote mbili.
Pia mkuu wa mkoa
aliiagiza familia hiyo kutaftiwa nyumba ya kuishi ifikapo kesho ili iweze
kupata makazi ya muda wakati ikiendelea na maandalizi ya kujenga makazi yake
mapya ya kudumu baada ya kupokea fidia akisema hatua hiyo ni muhimu kwa usalama
wa familia hiyo pamoja na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendelea bila
kuathiri maisha ya wananchi.
Itakumbukwa kuwa Julai 4, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Suguti, familia ya Mzee Ruhumbika Machumu iliwasilisha kero yao kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakieleza kuwa shughuli za uchimbaji zinazofanyika karibu na makazi yao zimekuwa zikisababisha usumbufu mkubwa ikiwemo kelele pamoja na mawe kurushwa kuelekea kwenye nyumba zao wakati wa shughuli za uchimbaji.
Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Mkuu alielekeza kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji katika eneo husika hadi pale mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu utakaolinda maslahi ya wananchi na kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea kwa amani na usalama.
Hatua ya Mkuu wa Mkoa ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo inatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha migogoro kati ya wananchi na wawekezaji inatatuliwa kwa njia ya mazungumzo, huku haki za kila upande zikizingatiwa kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.
Aidha kufutia
maelekezo hayo familia hiyo imeridhia kupokea kikasi cha shilingi Milioni 40
ilikupisha katika eneo hilo jambo lilokubaliwa na pande zote mbili.