MBUNGE MUSOMA MJINI AIOMBA SERIKALI KUANZA MCHAKATO UJENZI WA BANDARI YA MUSOMA
Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini Mgore Miraji Kigera ameiomba serikali kupitia wizara ya Uchukuzi kuanza mchakato wa ujezi wa bandari ya Musoma ili kufungua fursa za uchumi kwa mkoa huo kwa kuunganisha na nchi za Kenya na Uganda.
Ombi hilo limetolewa mjini Musoma leo Februari 23,2026 na Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini kwa Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa
alipofanya ziara mkoani Mara kwaajili ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara yake.
Mgore alisema amesema bandari hiyo itachangia uwepo wa matokeo chanya katika sekta ya uchumi hasa ikiunganishwa na uwepo reli ya SGR inayotarajiwa kujengwa kutoka Tanga- Arusha hadi Musoma.
kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans
amefafanua ujenzi wa bandari hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya 2025/50 sambamba na ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2025/30.
"Usafiri wa majini ni rahisi na utasaidia kupunguza gharama za bidhaa lakini pia utasaidia kuunganisha fursa za kiuchumi na biashara kwa mkoa wetu na nchi za Kenya na Uganda ambapo wafanyabiashara watakuwa na uwezo na njia rahisi ya kusafirisha bidhaa kati ya nchi hizo na mkoa wetu," amesema Kanali Mtambi
Kuhusu uwanja wa ndege wa Musoma Kanali Mtambi ameiomba Serikali kuanzisha safari za ndege katika uwanja huo kwenda Mwanza, Dodoma na Dar es salaam ili kurahisisha masuala ya usafiri na usafirishaji kutoka mkoani humo.
Mbunge wa Musoma Mjini,Mgore Miraji amesema bandari ya Musoma iliacha kufanyakazi kwa zaidi ya miaka 20 na kwamba bandari hiyo ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa mji wa Musoma na watu wake.
Amesema bandari hiyo inapaswa kufufuliwa na ianze kufanyakazi ili kuunufaisha mkoa na watu wake.
Amesema kutokana na serikali kutumia fedha nyingi kwaajili ya ujenzi wa meli ndani ya ziwa Victoria meli hizo zinatakiwa kufanya safari katika mji wa Musoma pia na kuunganisha na miji mingine ikiwepo mji wa Kisumu nchini Kenya.
Akizungumzia ombi hilo, Profesa Mbarawa amesema wiazara yake inatarajia kutuma wataalamu kwaajili ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuruhusu mchakato wa ujenzi kuanza.
Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bandari za Mwanza, Bukoba na Kemondo hivi sasa ni zamu ya ujenzi wa bandari ya Musoma.
"Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta hii ya uchukuzi ili kufungua uchumi wa mikoa yote kupitia usafiri wa anga,majini,barabara hivyo suala la ujenzi wa bandari ya Musoma ni jambo la lazima na tutahakikisha bandari inaanza kutumika ndani ya miaka hii mitano," amesema
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Ezra Daniel amesema ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma hivi sasa umefikia asilimia 60 za ujenzi wake.
Amesema uwanja huo wenye urefu wa kilomita 1.705 unataajiwa kugharimu zaidi ya Sh36.3 bilioni na kwamba utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kupokea ndege za kati tofauati na sasa ambapo uwanja huo unapokea ndege ndogo.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Musoma wamesema kusimama kwa bandari ya Musoma kwa namna moja ama nyingine kumerudisha nyuma maendeleo ya wakazi wa mji huo hivyo ni vema bandari hiyo ikafufuliwa na kuanza kazi kara moja.
"Kufufuliwa kwa bandari hii kutachochea ukuaji wa Uchumi ndani ya mji wetu Mkoa na taifa kwa ujumla, uchuni wa mtu nmoja nmoja utakuwa sambamba na wa mkoa na wilaya pia," amesema Rajabu Karangi.