M23 YAITAKA CONGO KUTOINGIZA SIASA KATIKA VIFO VYA WACHIMBA MIGODI RUBAYA
Waasi wa kundi la M23, wameishtumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa kugeuza vifo vya wachimba migodi kuwa suala la kisiasa.
Mwisho wa wiki iliyopita, watu mia mbili walifariki eneo la Rubaya nchini DRC baada ya kuporomoka kwa mgodi mmoja eneo hilo.
Katika taarifa yao, kundi la waasi la M23, limesema kuwa serikali ya Kinshasa inakwepa majukumu ya kuwajibikia vifo hivyo kutokana na utepetevu wao.
Msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka, alisema kumekuwa na vifo vingi ambavyo vimetokana na migodi kuporomoka hapo awali, ila idadi kamili ya waliofariki bado haijulikani, na bado serikali haijashughulikia suala la usalama wa migodi.
“Badala ya kufanya swala hili kuwa la kisiasa, serikali inafaa kushughulikia mapungufu yake.” alisema Kanyuka.
Kundi hilo linasema vifo katika migodi ya Rubaya, vilitokana na maporomoko ya ardhi, baada ya mvua kubwa kunyesha na kusema kuwa watasimamia matibabu ya waliojeruhiwa.
Kundi la waasi wa M23, liliuteka mji wa Rubaya mwaka wa 2024 na wamekuwa wakisimamia shughuli za kuchimba madini eneo hilo, licha ya serikali kupiga marufuku.
Juhudi za kudumisha amani mashariki mwa DRC bado hazijafua dafu, kutokana na mivutano kati ya makundi yaliyojihami na serikali ya taifa hilo.
