WANAFUNZI WATOROKA WAKIDAI KUKWEPA VIBOKO NA NYAYA ZA UMEME .
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ndolage, Frederick Byarugaba alisema wanafunzi hao (majina tunayahifadhi) walitoka nyumbani kwao Kitongoji cha Buganda B, Kamachumu na walipata usafiri wa kuelekea Bukoba Mjini.
“Baada ya taarifa hizo kusambaa kuwa wanafunzi wametoroka, uongozi wa shule ulitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, Kituo cha Kamachumu, Muleba,” alisema Byarugaba.
Alisema watoto hao walionekana kwa mara ya kwanza, Manispaa ya Bukoba wakitembea pamoja na baadhi ya watu wakiwamo abiria waliwakamata na kutoa taarifa polisi na kwa uongozi wa shule.
“Walikuwa na utoro wa rejareja na mara kadhaa wamekuwa wakikanywa kuhusu tabia mbaya ya utoro, hivyo baada ya wazazi kutoa taarifa ya kutoonekana nyumbani tulianza kusambaza ujumbe wa kuwatafuta,” alisema Byarugaba.
Mmoja wa walezi wa watoto hao, Christopher Kalumuna alisema kuwa baada ya mwalimu wa zamu kudai hawakuonekana shuleni hapo alisambaza taarifa kwenye miji midogo ya Kemondo, Kyetema na Bukoba Mjini hadi kwenye vituo vya magari ili kubaini kama wanaweza kusafiri.
“Huyu ni mtoto wa marehemu kaka yangu (jina tunalihifadhi) na mama yake naye ni marehemu, alikuwa akinifanyia kazi za nyumbani baada ya kutoka shule,” alisema Kalumuna.
Akizungumza kuhusu kilichowafanya kutoroka, mtoto huyo alisema walirubuniwa na mwenzao, ambaye aliiwambia kuwa shuleni kumeandaliwa adhabu ya watoto watoro hivyo watoroke kuepuka viboko au nyaya za umeme.
“Tuliogopa adhabu na ni kweli tumekuwa
watoro kila mara na tunachelewa shule. Tulipoondoka tulilala kichakani
bila kula huko Kemondo na tulitembea kwa miguu.
“Baada ya kufika Bukoba mjini kiongozi
wetu (mwanafunzi mwenzao) alitutoroka na tuliokotwa baada ya kuanza
kulia, ndipo tukamweleza aliyetuokota akatupandisha kwenye gari hadi
Kamachumu,” alisema mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Agustino Olomi alithibitisha kupokea taarifa za watoto hao.
Na Shaaban Ndyamukama, Mwananchi