SIKU YA WANAWAKE YAADHIMISHWA KIPEKEE MUSOMA VIJIJIN.
Baadhi
ya akinamama waliojitokeza kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya
Wanawake duniani zilizofanyika kwenye kijiji cha Bwai Kumsoma, Jimbo la
Musoma vjijini.
MAADHIMISHO ya siku ya wanawake duniani Jimbo la
Musoma vijijini yameadhimishwa kwenye kijiji cha Bwai Kumsoma kwa
kufanyika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza kwenye sherehe hizo mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya
ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney aliwataka wanafunzi wa kike wa shule
ya msingi Bwai kusoma kwa bidii ili wakabiliane na vitendo vya ukatili
kwa watoto wa kike kwa kuzitambua haki zao.
Dkt. Naano alisema, Serikali inaendelea na jukumu lake la kumlinda
na kutetea haki ya mtoto wa kike ili aweze kutimiza malengo aliyojiwekea
bila kujali itikadi za kisiasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Musoma Flora
Yongolo alisema, lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza mshikamano wa
wanawake na kuhimiza mapambano dhidi ya ukatili wa mtoto wa kike ili
kutimiza malengo ya kufikia kwenye uchumi wa kati.
Mkurugenzi huyo alisema, kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kudhibiti
baadhi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya mwanamke kwenye
jamii za vijijini, ingawa jitihada zaidi zinahitajika ili kutokomeza
kabisa vitendo hivyo.
Akieleza jukumu la Serikali kwa kushirikiana na vitengo vya haki za
binadamu alisema, wameendelea kutoa ushirikiano hasa kwenye usawa wa
kijinsia na kumuwezesha mwanamke kisiasa, kiuchumi, kielimu na kiafya
ili aweze kufikia malengo.
Mkurugenzi Yongolo aliendelea kusema, katika uundaji wa majukwaa ya
kuwawezesha wanawake kiuchumi, wametoa elimu kwa vikundi vya wanawake
vinavyojishughulisha na ushonaji, ubunifu, ujasiliamali kwa kutengeneza
vitu vya asili na makundi mengine ya wanawake.
Aidha, Yongolo aliwataka akina mama kujikita zaidi kwenye kilimo cha
umwagiliaji ili kujiinua kiuchumi ambapo vikundi vya akinamama kutoka
vijiji vya Suguti, Lyasembe, Nyambono na Mugango vilikabidhiwa mashine
za umwagiliaji.
Mbali na mashine hizo, katika maadhimisho hayo shilingi milioni 23
zilitolewa kwa vikundi 10 vya akina mama na vijana kwa ajili
kujiendeleza katika shughuli za kilimo na biashara.
Vikundi vilivyopokea fedha hizo ni Kikundi cha akinamama cha
Mshikamano, We grow, Jitahidi ufaidike, Nyakabhungo, Juhudi, Jaribu,
Bomafa, Amani na Upendo na kikundi cha Karpentas.
Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo
aliungana na akinamama kuadhimisha kilele cha siku ya wanawake duniani
kwa kutoa mchango wa miche ya miti ili kuwahamasisha watoto wa kike
kulinda mazingira ambapo katika sherehe hizo miti 3,000 ilipandwa kwenye
shule ya Msingi Bwai.
Prof. Muhongo pia alitoa mabati 54 kwa kikundi cha wanawake wa kijiji
cha Bwai Kumsoma (We grow) kwa ajili ya kuezeka vyumba vya madarasa
vilivyojengwa na kikundi hicho.