WANANCHI NYASAUNGU WARUDISHA NGUVU KUJENGA ZAHANATI YAO.



Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nyasaungu wakifuatilia kwa makini mkutano wa kujadili kuanza upya kwa ujenzi wa zahanati ya kijiji chao ambao ulisimama kwa miaka mingi.



wananchi wakifatilia kwa makini katika mkutano wa maendeleo





Na Mwandishi Wetu
BAADA ya kusimama kwa muda mrefu bila kuendeleza ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Nyasaungu, Jimbo la Musoma vijijini, wananchi wa kijiji hicho wamerudi kwa nguvu mpya ya kupanga mikakati ya kuendelea na ujenzi wa zahanati hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa na wananchi wa kijiji hicho mara baada ya kutolewa taarifa kwamba, changamoto zilizokuwa zinakwamisha ujenzi huo uliosimama kwa takribani miaka 12 zinatafutiwa ufumbuzi na hivyo ujenzi unatakiwa kuendelea.


Tayari ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini imekutana na Mganga Mkuu wa wilaya ya Musoma na kupata ufumbuzi wa changamoto hizo na kuwataka wananchi wa kijiji cha Nyasaungu kuungana pamoja kwa kushirikiana na viongozi wao ili kufanikisha huduma ya afya katika kijiji chao.

Kwa upande wao, wananchi wa kijiji hicho kwa kauli ya pamoja wamekubali kuendeleza zoezi hilo haraka iwezekanavyo na kuungana na Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo ili kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo.

Wananchi hao wamewaomba viongozi wao wa serikali ya kijiji wakae mapema kwa ajili ya kupanga bajeti na kuirudisha kwao kwa ajili ya kuanza michango na shughuli nyingine ndani ya wiki hii ili kuharakisha ujenzi huo.


Naye Diwani wa kata ya Ifulifu Rashidi Meru kwa niaba ya wananchi wa kata ya Ifulifu na kijiji cha Nyasaungu, ameipongeza ofisi ya Mbunge kwa kuona umuhimu wa kuwa na zahanati katika kijiji cha Nyasaungu na kuungana na wananchi wa kijiji chake katika kufanikisha zoezi la ujenzi huo.
Powered by Blogger.