MKUU WA MKOA WA MARA AZITAKA HALMASHAURI KUSIMAMIA FEDHA ZA RUZUKU ZINAZOTOLEWA NA AGPAHI.
Mkuu wa mkoa wa mara Mh.Adamu Malima (aliyesimama) akitoa maagizo kwa viongozi wa mkoa mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa mbalimbali za mkoa huo katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa. kushoto kwake ni Dc wa musoma, Dr.vicent Naano na kulia kwake ni kaimu katibu tawala mkoa Josephati Nyanda.

Meneja wa AGPAHI kanda ya Ziwa Dr.Nkingwa Mabelele akiwasilisha taarifa katika kikao cha (RCC )
Sehemu ya viongozi wa ulinzi na usalama wakifatilia kikao cha ushauri cha mkoa(RCC).
sehemu ya wajumbe wakiwa katika kikao .
Mkuu wa wilaya ya Tarime,Glorious Luoga(kushoto) akiwa na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu(aliyeshika mikono) kwenye kikao hicho .
Viongozi wa dini wakiwa kwenye kikao hicho .

Mganga Mkuuu wa mkoa wa Mara Dr. Francis mwanisi akiwasilisha taarifa katika kikao cha ushauri( RCC)
Serikali mkoani Mara imesema itashirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayotekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo mkoani humo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima wakati wa kikao cha ushauri wa Mkoa wa Mara (RCC) kilichofanyika katika Manispaa ya Musoma ambapo aliweka wazi kushirikiana na shirika la AGPAHI ,ambalo hujishughulisha na mapambano ya Virusi vya Ukimwi.
Pia Malima aliziagiza halmshauri zote Mkoani humo kupitia Wakurugenzi kuhakikisha kuwa zinatoa ushirikiano wa matumizi bora wa ruzuku za ukarabati wa Zahanati zinazotolewa na AGPAHI kuzisimamia ipasavyo fedha hizo.
" Simamieni fedha hizi mnaona sisi hapa tunashikana mashati ilikupata sh, 20 bilioni kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa hospitali ya Mwalimu Nyerere, lakini hawa wanatoa fedha nyingi kwa mkupuo, tusiwakatishe tamaa kwa kuchelewa kutuma taarifa ya utekelezaji wa fedha hizo," Malima alisisitiza.
Meneja wa AGPAHI kanda ya Ziwa Dr.Mabelele alisema shirika hilo linalenga dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi katika kutekeleza miradi yake kwenye mikoa saba ya Geita,Mara, Manyara, Mwanza,Shinyanga,Simiyu na Tanga.
Katika mkoa wa Mara shirika la AGPAHI linatekeleza mradi wa 'Boresha' ambao sasa umeonekana kuwa na manufaa katika maeneo yote unakotekelezwa.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi huo katika kikao cha RCC, Dr. Nkingwa alisema mradi wa Boresha ni wa miaka mitano na ulianza kutekelezwa mwaka 2016 utakamilika mwaka 2021.
Aliongeza kuwa fedha za ruzuku zinazotolewa husaidia kuratibu shughuli mbalimbali za Ukimwi ili kuboresha utoaji huduma bora za Afya, kusaidia Halmashauri kufanya usimamizi na ufatiliaji wa utoaji wa huduma hizo katika maeneo husika.
"Vituo vya afya vimefamikiwa kununua vifaa vya tiba ikiwemo vya kuangalia ongezeko la Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa mwathirika," alisema Nkingwa.
Kwa kipindi cha Oktoba 2016 hadi Septemba 2017 Shirika la AGPAHI limetoa huduma ya kupima afya ya watu 199,889 na kati ya hao 7325 walikutwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU).
Mganga mkuu wa mkoa wa Mara, Dkt.Francis Mwanisi alishauri mkoa wa Mara kuunga mkono ushirika wa AGPAHI kutokana na ushirikiano wake ulioonyeshwa katika maeneo ya mradi kwa kuwa umekuwa msaada kwa sehemu kubwa za huduma ya afya katika vituo vya afya mkoani Mara.
Kwa upande, mkuu wa Wilaya ya Musoma Dr.Vicent Naano, aliliomba shirika la AGPAHI kuzishirikisha Halmashauri wakati wa upangaji wa ruzuku za miradi kutekelezwa kwani itasaidia kuondoa changamoto ya halmashauri kurudia kutenga fedha katika vituo hivyo